Pages

Pages

Tuesday, April 02, 2013

Waandishi wa Habari za Michezo watolewa kamasi na wazee Zanzibar



Katibu Mkuu wa TASWA Taifa, Amir Mhando
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
TIMU ya Soka ya Waandishi wa Habari za Michezo Zanzibar (TASWA
Zanzibar) juzi ililazimishwa sare ya kufungana mabao 4-4 na timu ya wazee
wa Zanzibar ‘Zanzibar Veteran’ katika mchezo wa kirafiki uliochezwa
Amaan na kufurahisha watu wengi.

Mchezo huo ambao ni mjumuisho wa michezo ya wiki ya Pasaka ulichezwa
ukiwa na ushindani wa hali ya juu kwa kila upande kutaka kuondoka na
ushindi uwanjani hapo, huku wazee hao wakionyesha soka la uhakika na kuacha watu midomo wazi.


Ingawa waandishi ndio waliotangulia kupata bao kwa Mohammed Saleh dakika ya sita tu ya mchezo huo, lakini wazee walisawazisha dakika ya 9 na mchezaji wake Mwinyi Haji Fido.

Kuingia kwa mabao hayo kulizidisha kasi ya mashambulizi kwa pande zote
mbili wakati huku Veteran hao waliokuwa wakionesha soka la kizamani na
la ufundi wakaweza kuongeza bao la pili katika dakika ya 24
lililofungwa na Haidar Abbas wakati bao la tatu likifungwa katika
dakika ya 27 na Mohammed Abbas.

TASWA baada ya kuona wameshatangulia kwa mabao hayo waliongeza kasi ya mashambulizi langoni kwa wazee hao na kufanikiwa kupata bao la pili
katika dakika ya 31 lililofungwa na Mohammed Kassim na kuifanya miamba hiyo iende mapumziko wakiwa Taswa mabao mawili na Veteran mabao matatu kwa ajili ya kujipanga na kurejea uwanjani wakiwa na nguvu mpya katika mchezo huo wa aina yake.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu ya Waandishi wa habari ambayo iliwatoa wachezaji wake Ali Khamis,
Yahya Saleh na Mohammed Kassim na nafasi zao kuchukuliwa na Ikram
Omar, Jamal Ali na Kombo Ali.
Safu hiyo iliweza kubadilisha hali ya matokeo na
kufanikiwa kusawazisha bao la tatu katika dakika ya 55 lililofungwa na
Kombo Ali huku bao la nne likifungwa na Ikram Omar katika dakika ya
75.

Zanzibar veteran baada ya kuona upepo umewageukia walianza kuleta
mashambulizi ya kasi langoni kwa wapinzani wao na kufanya mabadiliko
ya kuwatoa wachezaji wake mabadiliko ambayo yaliwafanya waweze
kusawazisha bao la nne lililofunga na Abdallah Ali ‘Teacher’ na
kuufanya mchezo huo umalizike kwa sare ya mabao 4-4.

Katika wiki iliyopita timu ya Taswa FC iliweza kuifunga timu ya Women
fighter iliyokuwa na wachezaji mchanganyiko wakiwemo wanaume na
wanawake mabao 3-1 huku mchezo wa kwanza wakifungwa na wawakilishi
mabao 3-2.

No comments:

Post a Comment