Pages

Pages

Saturday, April 06, 2013

Vitanda vinajua siri nyingi za wapendanao



MAMBO FULANI MUHIMU
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
UKIONA watu wanatembea asubuhi au tunapokutana nao maofisini, ujuwe kuwa si wote wanafurahia uhusiano wao au ndoa kwa wale waliobarikiwa jambo hilo, zaidi ya maumivu na kilio kila wakati.
Diamond na Wema Sepetu enzi za upendo wao
Wapo watu ambao kila muda wa kurudi majumbani mwao unapofika, hakika wanatamani wakati urudi nyuma ili waendelee kukaa maofisini mwao.

Aidha, kwakuwa hilo haliwezekani, basi wanaona suluhu kubwa ya kutuliza akili zao ni kukimbilia kwenye vijiwe vya kahawa au pombe na kukaa hadi usiku wa manane.

Haya ni mambo ya ajabu sana. Huwatokea watu wengi katika uhusiano, hasa wale mapenzi yanayowajia kwa upande wenye karaha na machungu ya aina yake.

Wapo watu katika mapenzi ni wasumbufu sana. Hao hawataki kujua kuwa wapenzi wao, wachumba au wana ndoa wao wameamua kutulia na wao.

Kwasababu ya kushindwa kufahamu walau robo ya upendo wa wenzao, wameamua kufanya vituko, hivyo kuwa njia ya wenzao kutamani kuwa mbali nao.

Haya si mambo mazuri katika suala zima la uhusiano wa kimapenzi, hivyo wadau tunatakiwa tulijuwe hilo kwa faida ya wapenzi wetu kwa ujumla.

Uhusiano ambao hauna maelewano, huo hauwezi kuwa na mashiko wala kuendelea kuchanua. Tutakuwa na uhusiano wenye mashaka makubwa.

Tutazalisha watu wanaotamani kutoka nje ya ndoa kwasababu sisi tuliokuwa nao hatuwavutii au hatufanyi mambo ambayo wao yanawafarahisha.

Kwasababu hiyo, ndio maana wapo watu ambao licha ya kujiita wapo kwenye ndoa, lakini hawajawahi kugusana na wana ndoa wenzao kwa kipindi hata cha miezi sita kama sio mwaka.

Wana ndoa hao huishi kama mtu na dada yake au mama yake mkwe. Huyu amelala kule na mwingine yupo upande ule. Tena kama kitanda ni cha futi sita kuendelea ndio balaa.

Nani amuanze mwenzake. Uchokozi hapo hauruhusiwi. Mmoja akijitia kukosea na kumgusa mwenzake kwa bahati mbaya, huenda matusi yakaporomoshwa.

Hayo ni mambo ya kushangaza na kuogopesha kupita kiasi, maana licha ya watu kuwa kwenye ndoa, lakini hawaishi kama wana ndoa.

Ndio maana hapo mwanzo wa mada hii nilisema kuwa vitanda vinajua vitu vingi mno vya wanandoa. Huo ndio ukweli wa mambo.

Kuna msomaji wangu mmoja aliandikia meseji kuwa yeye anateswa na mume wake. Dada huyo akasema ameamua kumuacha kama alivyo.

Kama hivyo ndivyo, ina maana hakuna hata kupeana haki ya ndoa? Kwa mtindo huo, bado tutaajita ni wana ndoa? Haya ni mambo yaliyoenea kwa wana ndoa wengi.

Kwa kulijua hilo, nadhani kila mmoja ajaribu kuangalia kwa wakati gani anatumia kufanikisha ulinzi wa ndoa yake, uchumba au uhusiano wake.

Kila mmoja ajaribu kufumba macho japo kwa dakika moja kufikiri alipotoka na mtu wake pamoja na kuombea dua uhusiano wake kwa faida ya mtu wake.

Kama hujawahi kuugusa mwili wa mke, mume wako kwa kipindi kirefu sasa, leo iwe mwisho na mwanzo upya wa kuusalimu kadri ya uwezo na ujuzi wako.

Ushike mkono wa mtu wako. Upeleke mdomoni mwako kwa njia ya upendo, ukiutaka radhi baada ya kuukosa kwa kipindi ambacho kitendo kama hicho kukifanya kilikuwa ni agharabu

Katika suala la migogoro ya kimapenzi, wakati mwingine kunakuwa hakuna sababu inayoonyesha chanzo zaidi ya ujana, utoto na kutokujua njia nzuri za kulinda uhusiano huo, hivyo naamini ni wakati wetu sasa kulinda, kuthamini na kuona tuna kila sababu ya kuheshimu watu wetu kwa faida ya uhusiano wetu na kuacha kasumba zetu.
0712 053949
0753 806087

No comments:

Post a Comment