Pages

Pages

Friday, April 26, 2013

SHEREHE ZA MUUNGANO



Tukubali ufa wa muungano na tuurekebishe

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KUMEKUWA na maneno makali kutoka kwa baadhi ya wanaojiita wanaharakati, wakitaka kuvunjwa kwa Muungano wa Tanzania Bara na Visiwani.
                       RAIS wa Tanzania, Jakaya Kikwete
Katika kuhaharalisha mahitaji yao, watu hao wamekuwa wakiorodhesha mambo kadhaa, wakionyesha kuwa ndio chanzo cha kuutoa uhai muungano huo ulioingiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambao kwa sasa ni marehemu.

Muungano huo uliingiwa rasmi Aprili 26 mwaka 1964 na kushuhudia Bara na visiwani ikiwa ni nchi moja yenye mpangalio thabiti wa kiutawala.

Hata hivyo, wataalamu wa mambo wanasema kuwa tangu siku ya kwanza ya Muungano huo, kero kadhaa zilianza kujitokeza na kukua hadi leo hii ambapo tunahushudia watu wakiupinga muungano huo.

Katika kuujadili muungano huo, mambo mengi mabaya yanatokea, yakiwamo aina ya wananchi wanaoishi kwa upande wa Bara na Visiwani pamoja na fursa sawa za ajira kwa sehemu hizi za muungano.

Unapozungumzia muungano unaelezea sehemu mbili zinazofanya kazi kwa pamoja kwa makubaliano maalumu. Kama hivyo ndivyo, mmoja wapo anapokwenda kinyume, ni wazi anahitaji kuambiwa ukweli kama nia ni kuufanya Muungana huo uendelee kuwa na mashiko.

Kwa mfano, nimekuwa nikichanganywa mno na malalamiko ya wafanyabiashara wanapolalamikia kutozwa kodi pande zote mbili za Muungano. Mtu anaponunua bidhaa Dar es Salaam na kulipa kodi, sidhani kama huyo anahitaji tena kulipia anapoingia Bandari ya Zanzibar.

Hali kazalka anapolipia kodi Zanzibar, si sahihi tena kumtoza kodi anapoingia Dar es Salaam au sehemu yoyote ya Tanzania Bara, ukizingatia kuwa hizi ni nchi mbili zilizoungana.

Mbali na kero hizo ambazo zinasababisha malumbano kutoka kwa watu wengi, pia zipo kero nyingine kama vile mambo ambayo wenyewe wameyaita si ya Muungano.

Haya ukiyapigia hesabu unabaki kinywa wazi.  Na ndio maana katika kunyamazisha wale wanaopigia kelele muungano huu, serikali za Ban a Visiwani zimekuwa zikitumia nguvu kubwa, ikiwapo kuwanyamazisha watu katika kuelekea kuipata Katiba Mpya kwa kuweka kipengele kisichoruhusu kuujadili Muungano huo wa Bara na Visiwani.

Sidhani kama hapa tunajenga. Zaidi tunazidisha malumbano yasiyokuwa na msingi kwa namna moja ama nyingine. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shain mapema mwaka huu aliwatoa hofu wanaohoji kutokuwepo kwa hati halisi ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kusema hati hiyo ipo na iwapo hawaamini watu hao waende Umoja wa Mataifa New York.

Shein aliyasema hayo akiamini kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni chimbuko la kuasisiwa kwake kulitokana na ridhaa ya wananchi wa pande mbili za Muungano.

Kwa mujibu wa Shein, faida za Muungano ni kubwa kwa upande wa Zanzibar, akielezea kutapakaa kwa watu hao katikaa mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara pamoja na kupewa fursa nyingi za uwekezaji.

Hili ni jambo sahihi na limezungumzwa wakati ambapo baadhi yao wanajaribu kupitisha hoja za kusambaratika muungano huo, ukikumbuka kuwa hapo kabla ilikuwa ikiagiza bidhaa za vyakula na mahitaji mengine kutoka nchi za Pakistan, Japan na mashariki ya mbali; ambapo kwa bahati nzuri vitu hivyo vipo.

Nadhani katika kuliangalia suala zima la Muungano, kila Mtanzania bila kuangalia anatokea Bara au Visiwani, ni vyema akajaribu kuhakikisha kuwa anakuwa na uchu wa kuulinda Muungano huo au kuukosoa kwa ajili ya kuufanya uendelee kuwapo.

Wengi tunajua kuwa kuwapo kwa Muungano huo ndio sababu ya Visiwa vya Unguja na Pemba kujiona ni kitu kimoja, hivyo siku Muungano utakaposambaratika, hakika kitakachofuata ni uchochezi usiokwisha kwa visiwa hivyo.

Angalia, ingawa watu wengi wa Zanzibar wamekuwa wakilalamika mizengwe inayofanywa na upaande wa Bara, hasa pale kulazimishwa kukubali kuongozwa na watu ambao ndugu zao wa Tanzania Bara wanawaona wanaofaa kushika hatamu za uongozi visiwani.

Hili ni tusi kubwa, likiangaliwa kuwa limetokana na dharau kwa upande wa watu wa Zanzibar kuwa hawajui kuchagua machaguo mazuri kwa ajili ya kuwaongoza, hivyo kusababisha upande wa Bara kuingilia kila jambo.

Suala hilo ndilo linalozidisha malumbano ya kuungalia Muungano huo wenye ufa na uliopoteza thamani, hasa kwa vitendo vya kuwaamulia mambo, hata kama wananchi wenyewe wana haki hiyo ya kuchagua kwa faida yao.

Tuyaseme haya hata kama tutaitwa majina mabaya ya kukatisha tamaa, ukizingatia kuwa ndio msingi imara na utakaoweka suluhu ya kuulinda Muungano, leo ambapo Watanzania tupo kwenye mchakato wa kuipata Katiba Mpya.

Tusipokuwa makini, Muungano utakufa. Utakufa, maana Wazanzibar wameinuka na wanahitaji haki zao ambazo kwa miaka kadhaa wamekuwa wepesi kudai kuwa zinakandamizwa na upande mwingine wa shilingi, yani Tanzania Bara.

Kwa bahati nzuri, haki hii ya Wazanzibar inadaiwa kwa sauti moja, yani nguvu ya umma, hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kufanikiwa, hasa kama kero zinazotajwa hazijapatiwa ufumbuzi kwa namna moja ama nyingine.

Wapo baadhi ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Visiwani humo wamekuwa wakihitaji mno kuchagua wenyewe Rais wao bila kuingiliwa na upande wa Bara, wakijua kuwa hilo ndilo jawabu la kujiamulia mambo yao.

Je haya si mambo yanayopandikiza zaidi chokochoko za kuuvunja Muungano hasa kama hazitapatiwa ufumbuzi. Najua kuwa baadhi ya viongozi wa serikali na vyama pia ni wagumu kuchukua ushauri au kukubali kukosolewa.

Suala kama hili sit u halitakiwi kuachwa kama lilivyo, bali linahitaji vikao sahihi, ukizingatia kuwa chama ndicho kinachotoa rais, haijalishi kuwa anatokea CCM au Chama Cha Wananchi CUF kwa upande wa Zanzibar.

Kila mtu anajua kuwa Muungano wa Bara na Visiwani ni pamoja na kupokezana nafasi ya uongozi wa juu, yani Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo kwa sasa upo chini ya Jakaya Mrisho Kikwete.

Kikwete alipokea kijiti kutoka kwa Rais wa Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin William Mkapa. Hatujui lini utaratibu wa kuachiana nafasi za urais uliachwa na kuzidisha chuki za Muungano.

Ukiliuliza swali kwa viongozi wa juu wa CCM, watakwambia hayo yanazungumzika, ajabu ni kuwa jibu hilo litaendelea kutolewa kila siku, maana ni ngumu kukaa kulizungumzia kwa faida ya Muungano huo.

Haya na mengine mengi yanaibua minong’ono kuwa Muungano hauna faida. Ingawa upande wa serikali wanaona kuna faida kubwa kuendelea kuwapo kwenye Muunganao, lakini wananchi baadhi yao hawataki.

Kwa bahati nzuri, hata waliokuwa upande wa Bara, ukiwauliza juu ya Muungano wanaweza kukwambia uvunjwe au upitiwe upya na kuangalia faida zinazoweza kupatikana kwa sehemu zote mbili na kuepuka malumbano yanayotokea.

Ukimya wa serikali hauwezi kuwa na tija. Ndio maana baadhi ya wananchi kutoka Bara wanaona Zanzibar si sehemu nzuri ya kuishi kutokana na baadhi yao kufanya vitendo vya fujo hadharani hasa kwa watu ambao si wazaliwa wa Visiwani.

Vitu kama vile makanisa yanachomwa au kufanyiwa fujo, hivyo endapo serikali bado haitakuwa na mipango ya kuweka sawa ufa wa muungano, hakika hatari zaidi inaweza kutokea na kuiweka nchi kwenye wakati mgumu.

Kwa sababu hiyo, ni vyema watu wote tukaendelea kujifunza kuwa kero (au malalamiko) ya Muungano hayapo tu katika mfumo na uendeshaji wa shughuli za Serikali ya Muungano, bali hata ndani ya chama tawala cha CCM.

Hivyo upo umuhimu mkubwa kwa mfumo wa Muungano ukaangaliwa upya na kwa upana na urefu kwa sababu kila kukicha malalamiko yanazidi kuwa mengi, ingawa waheshimiwa wanajifanya hawaoni.

Licha ya kujifanya hawaoni, lakini Muungano ndio jambo linalogusa hisia za wengi hata kwenye mchakato wa Katiba Mpya hasa kwa upande wa Zanzibar, ambapo kila mtu anaonyesha kutoa hisia za kero zake juu ya Muungano huo.

Hivyo vyemaa tukatambua kuwa suala la kuwapo zamu ya urais kati ya Bara na Visiwani (hizi ni nchi mbili zilizoungana kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) nalo lisipuuzwe kwa kisingizio cha kwamba Zanzibar ni ndogo kama baadhi ya watu Bara, wakiwemo wabunge walivyojaribu kueleza katika kutaka malalamiko ya watu wa Visiwani yasitiliwe maanani, kitu kinachoweza kuzidisha machungu ya kuuvunja Muungano huu.

Ingawa wenyewe mara kadhaa hushindwa kuyasema haya hadharani kwa sababu wanazojua wenyewe ndani ya vyama vyao vya siasa, lakini wapo watu wanaolalama vichochocroni kuwa upande wa Bara hauwatendei haki na kwamba Muungano wa vyama vya ASP na TANU na kuunda CCM na wa serikali mbili (Zanzibar na Tanganyika) umekuwa ukisababisha watu wa Visiwani kuburuzwa.

Katika kulinda maslahi na uwepo wa Muungano, hakika litakuwa jamabo jema kama Tume ya Jaji Warioba itaziheshimu na kutozibana katika majumuisho yake kabla ya kuandikwa katiba mpya, hasa kwa wale waliofanikiwa kutoa hisia zao na maoni yao juu ya kero za Muungano kwa namna moja ama nyingine.

Tusipofanya hivyo, hatutaweza kuulinda Muungano huo hasa kama wananchi wenyewe wataendelea kuupinga, ingawa viongozi wataulinda kwa namna moja ama nyingine.
Mungu ibariki Tanzania.
babamkubwa@yahoo.com

No comments:

Post a Comment