Pages

Pages

Monday, April 08, 2013

Korogwe wawapigia magoti waamuzi wao wa soka

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
CHAMA cha Soka wilayani Korogwe (KRFA), kimewataka waamuzi wao wachezeshe kwa haki Ligi ya Gambo Cup inayoendelea, ili kuondoa malumbano na kupatikana mshindi wa haki kwenye michuano hiyo na hatimae kukuza kiwango cha michezo wilayani humo.
Mkuu wa Wilaya Korogwe, Mrisho Gambo na mdhamini wa Gambo Cup wilayani humo.

Mashindano hayo yanayoendelea wilayani Korogwe yamepangwa katika vituo nane, huku yakiandeshwa kwa udhamini wa Mkuu wa Wilaya Korogwe, Mrisho Gambo.

Akizungumza kwa njia ya simu, Mwenyekiti wa Chama hicho, Peter Juma, alisema kuwa kitendo cha kuwabana waamuzi wao kimetokana na kuhitaji ufanisi katika mashindano yao.

Alisema katika mashindano yoyote ya mpira wa miguu, waamuzi wana nafasi kubwa ya kuharibu au kujenga, hivyo wamejitahidi kuwaelimisha namna gani wanatakiwa wachezeshe kwa kufuata sheria za soka zilizopangwa.

“Tumekuwa tukizungumza na waamuzi mara kwa mara katika hali ya kuwajulisha namna gani wao ni muhimu na hawapaswi kuchezesha kwa matakwa ya watu fulani.

“Tunahitaji maendeleo ya michezo hasa mpira wa miguu, hivyo naamini tutafikia hatua nzuri na kuiweka wilaya yetu katika nafasi nzuri katika kiwango cha michezo,” alisema Juma.

Baadhi ya waamuzi wa soka nchini wamekuwa wakichezesha mechi huku wakilalamikiwa kuwa wanazindamiza baadhi ya timu, jambo linalosababisha Shirikisho la Soka nchini TFF kupiga kelele kuwakemea waamuzi hao.

No comments:

Post a Comment