Pages

Pages

Tuesday, March 05, 2013

Waziri Mkuu ataka watendaji wahamasishe vijana kufuga nyuki


Waziri mkuu Mizengo Pinda (mwenye miwani) akisaidiwa kutundika mzinga wa kisasa na naibu waziri wa mali asili na utalii Mh. Lazaro Nyalandu (kushoto) na mkuu wa mkoa wa Singida, Dk.Parseko Vicent Kone, kwenye maadhimisho ya utundikaji mizinga kitaifa uliofanyika katika kijiji cha Aghondo Manyoni Magharibi.

Waziri mkuu Mizengo Pinda, akihutubia kwenye kilele cha utundikaji mizinga kitaifa uliofanyika katika kijiji cha Aghondi jimbo la Manyoni magharibi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Uwekezaji na Uwezeshaji Dk.Mary Nagu, akitoa nasaha zake kwenye kilele cha utundikaji mizinga kitaifa uliofanyika katika kijiji cha Aghondi jimbo la Manyoni magharibi.(Picha zote na Nathaniel Limu).

Na Nathaniel Limu, Singida.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mizengo Pinda amewaagiza watendaji na viongozi mbalimbali, kuhamasisha vijana kujiunga/kuanzisha vikundi vya ufugaji nyuki ili waweze kupambana vema na umaskini pamoja na uhaba wa ajira.

Mh. Pinda ametoa agizo hilo wakati akizungumza kwenye kilele cha siku ya utundikaji mizinga kitaifa uliofanyika katika kijiji cha Aghondi jimbo la Manyoni Magharibi.
Amesema kazi ya ufugaji wa nyuki ni rahisi mno na ni tofauti na shughuli zingine za kiuchumi ikiwemo ya kilimo na ufugaji.

Waziri Mkuu amesema pamoja na urahisi huo, lakini ndiyo kazi nzuri ambayo ina uwezo mkubwa wa kumkomboa mhusika kiuchumi, kwa madai kwamba mazao ya ufugaji nyuki, yana soko zuri la uhakika wakati wote.

Mh. Pinda amesema kwa hali hiyo, upo umuhimu mkubwa kwa watendaji na viongozi kuhamasisha vijana  kwa bidii, ili waweze kujiunga katika vikundi na kwa njia hiyo watakuwa wamejijengea mazingira mazuri ya kuweza kupewa misaada mbalimbali ikiwemo ya kuwawezesha kufuga nyuki.

Katika hatua nyingine Waziri mkuu almesema ufugaji wa nyuki utasaidia sana kutunza mazingira na vyanzo vya maji.

Amesema kutokana na ukweli huo mazingira yakitunzwa vizuri na kulindwa pamoja na mambo mengine, nchi itarudi kwenye neema ya mvua zenye kheri.

No comments:

Post a Comment