Pages

Pages

Saturday, March 30, 2013

Unaijua Yanga au unaisikia, leo balaa Morogoro

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
TIMU ya Polisi Morogoro, leo itakuwa na kibarua kigumu mbele ya vinara wa ligi ya Tanzania Bara, Yanga SC, pale zitakapovaana katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, katika mfululizo wa mechi za Ligi hiyo inayodhaminiwa na Kampuni ya Vodacom Tanzania.
 Wachezaji wa Yanga wakijifua
Yanga inaingia uwanjani huku ikiwa kwenye nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa Bara kwa kujikusanyia jumla ya pointi 48, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 40, wakati Simba yenyewe ina pointi 34.


Mbali na Yanga na Polisi Morogoro, timu nyingine zinazoingia uwanjani leo ni pamoja na Simba watakaokuwa wageni wa Toto African ya jijini Mwanza, wakati Azam wenyewe wataingia uwanjani kucheza na Ruvu Shooting uwanja wa Chamaz, wakati Kagera Sugar watashuka uwanja wa Kaitaba kucheza na Mtibwa Sugar ya mjini Morogoro.

Timu zote tayari zimeshafika katika mikoa hiyo kwa ajili ya kuhakikisha kuwa wanatoka na ushindi, hali inayosababisha ushindani wa aina yake katika patashika hiyo ya Tanzania Bara.

Yanga, wamedhamiria kuifanyia umafia Polisi Morogoro kwa kuwatandika ili wajiweke kwenye naafsi ya kunyakua ubingwa wa Bara unaoshikiliwa na Simba, ambao mpaka sasa wameuweka rehani ubingwa huo.

Kocha wa Yanga, Ernest Brandit, ametangaza hali ya hatari kwa wapinzani wao, akisema kuwa lazima wawatandike wenyeji wao, Polisi Morogoro ili waunuse ubingwa na kuwapa shangwe mashabiki wao.

Kwa upande wa Simba, kocha msaidizi, Jamhuli Kihwelo Julio, alisema kuwa vijana wake wapo imara, ingawa kumekuwa na propaganda zinazofanywa ili kuwaweka kwenye wakati mgumu.

“Watu wanataka tuendelee kufanya vibaya kwa maslahi yao, lakini hakika vijana wapo imara na wana kila sababu ya kushinda mbele ya Toto African.

“Tumewasili jijini Mwanza tukiwa na ari kubwa, ingawa wapo waliozusha eti tumezuiwa kwa sababu wanazojua wenyewe na fitina zao,” alisema Julio.

Simba wanaingia uwanjani huku wakiwa na kumbukumbu ya kutoka Bukoba huku wakiwa wamefungwa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar.

Endapo Simba itafungwa na Toto leo, basi si tu itajiondoa kwenye ubingwa zaidi, bali hata ile nafasi ya pili itakuwa ngumu, kwa kuangalia mahesabu ya msimamo wa ligi, huku Yanga wao wakiwa kileleni kwa tofauti ya pointi 8 dhidi ya Azam yenye 48, huku Simba wao wakiwa na pointi 34.

Naye kocha wa Mtibwa Sugar, Mecky Mexime, alisema kuwa wamefika mkoani Kagera wakiwa na matumaini ya kuibuka na ushindi mbele ya Kagera Sugar, ingawa wanaamini mchezo utakuwa mgumu.

Kagera Sugar wenyewe wana pointi 34 sawa na Simba, wakati Coastal Union  na Mtibwa Sugar wamejikusanyia pointi 32 katika ligi ambayo imezidi kuwa na msisimko hasa nafasi za juu na chini, hasa zile zilizokuwa kwenye hatari ya kushuka daraja.

Mwisho

No comments:

Post a Comment