Pages

Pages

Sunday, March 03, 2013

Uchaguzi Mkuu Kenya 2013: Maandalizi yapamba moto


Na Dorine Otinga, Eldoret, Kenya
BILA shaka, zimesalia siku chache kabla ya uchaguzi mkuu wa kihistoria nchini Kenya ambao utafanyika Machi, 4 mwaka huu ikishuhudiwa wagombea nane wakichuana kuwania nafasi ya urais. Maandalizi kati ya wakenya dhidi ya uchaguzi yanafanywa kwa udi na ambari. Wanasiasa wanajaribu kushindani kila siku kwa kumwaga sera za kuwezeshwa kupata kura.

Kama nilivyoelezea juma lililokwishapita juu ya kura za maoni ya wananchi wa Kenya wanaosadiki wagombea wao. Nikumbushe tu, wakenya 328 walioulizwa kwenye zoezi la kura za maoni juu ya uchaguzi walikuwa na mitazamo mbalimbali.

Watu 92% wamekubali kuwa mdahalo kwa njia ya runinga ulisaidia kujua mbinu na uwezo wa kujieleza wa wagombea wao. Wengine 24% walilazimika kubadili mawazo yao kwa ajili ya wagombea waliodhani watawachagua. 

Wapigakura hawa 34% ina maana wamebadili mawazo kutoka kwa mgombea mmoja kwenda kwa mwingine. Wakenya 27% wanadhani Uhuru Kenyatta atashinda uchaguzi.

Wakenya 26% wanaamini Peter Kenneth atashinda kutokana na kufanya vizuri kwenye mdahalo. Vilevile 22% ya wakenya wanaamini Raila Odinga atashinda uchaguzi na yeye ndiye bingwa wa ushawishi hadi sasa akiwa na mgombea mwenza, Kalonzo Musyoka. 

Halafu kuna 12% wanapenda kuona Martha Karua akishinda kuchukua uongozi. Hata hivyo, kuna baadhi ya wakenya ambao hawajaamua iwapo watapiga kura au la. Waangalizi wa kimaitaifa wameshaanza kuwasilia hapa Kenya na wanatahadharisha ongozeko la watu watakaoacha kupiga kura.

Sababu zinazotolewa juu ya baadhi ya wakenya kuacha kupiga kura ni kutokana na yale machafuko ambayo yalitendeka mwaka wa 2007 na kusababisha maafa makubwa kwa wakenya. Wengi wao ni walioathiriwa na ghasia baada ya uchaguzi ambao wamekuwa na uchungu kutokana na mambo yaliyotokea baadaye, huku Uhuru Kenyatta na William Ruto wakifunguliwa mashtaka huko The Hague, nchini Uholanzi.

‘’Sisi tulifukuzwa shambani kwetu kule Molo, na tumeishi katika hema kwa muda wa miaka mitano.Tulijuta sana. Bado sijaamua iwapo nitapiga kura’’, alisema mwanamke mmoja aliyekuwa katika kambi ya wakimbizi. Ingawa serikali ilifanya juhudi ya kuwapa wakimbizi hawa mahali pa kuishi kwa muda na kukabiliana na maisha mapya yenye changamoto kubwa kuliko hali ile waliyozoea kabla ya machafuko.

Raila Odinga


Nje ya Kenya wetu wanadhani shamrashamra za siasa katika uchaguzi mkuu zimekuwa kwenye sura ya mdahalo na upigaji kura pekee. Lakini ukweli ni kwamba watpo watu wenye uchungu kwa hali iliyotokea.

Mpaka sasa hivi, bado wengi wao hawajaamua iwapo watapiga kura tena ifikapo Machi 4, licha ya wapigakura milioni 14.3 kuandikishwa na kupata sifa zote za kuchagua viongozi. Hili limekuwa kero kubwa kwa Tume huru ya Uchaguzi, na inaelekea Mkuu wa Tume hiyo, Isaac Hassan atakuwa na jukumu lingine kuwaelezea wakenya umuhimu wa kushiriki kikamilifu zoezi la kupiga kura.

Baadhi ya vituo vya habari vimeungana kwa nguvu kubwa sana na kuanzisha midahalo isaidiayo wakenya kujua ni kiongozi yupi atakayefaa kuchaguliwa ifikapo Machi 4. Juhudi hizi zimeongeza usikivu mkubwa sana kwa vituo vya habari, kwani vimefanya kazi ya kueneza uzalendo wa wakenya. 

Kulingana na mdahalo wa kwanza ambao ulihusishwa na runinga ya Citizen na vituo vingine, mgombea Mohamed Abduba  Dida, ambaye ni mgeni katika ulingo wa siasa aliweza kuinua umaarufu wake kutokana na uwezo wake wa kujieleza, kipaji chake cha kushawishi hadhira na vile vile ucheshi wake ambao uliamsha hisia za wananchi.

Raila odinga na Uhuru Kenyata walisalia maarufu zaidi kutokana na kuwa kwenye ulingo wa siasa. Mpaka sasa Odinga na Uhuru wanachuana vikali, huku taasisi za utafiti zikionyesha wanakaribiana sana kwa kujipatia ushindi. 

Mathalani, duru za kisiasa zinasema kwamba Uhuru Kenyatta na William Ruto hawatahudhuria mdahalo wa mwisho utakaofanyika kabla ya uchaguzi. Jambo hili limezua mjadala mkubwa hapa Kenya, ambapo wengi wanajiuliza kulikoni wasiweze kupanga njia za kufanikisha mdahalo badala yake wanakataa kuhudhuria?

Lakini kwa upande wao Uhuru na Ruto wanasema licha ya Changamoto ambazo zimewakumba, ikiwemo kesi katika mahakama ya ICC, wao wanaendeleza kampeni zao bila wasi wasi. Ilikuwa ni afueni kwao, baada ya Mahakama Kuu ya Kenya kusema kwamba, haiwezi kuwazuia kugombea kiti cha Urais, na kwamba uamuzi huo ungeweza kuamuliwa na Mahakama ya rufaa.    Akielezea sababu za kujitoa kwenye mdahalo wa mwisho, Uhuru Kenyatta alisema kuwa katika mdahalo uliomalizika hakutendewa haki hivyo haoni sababu za kushiriki tena.

Uhuru akielezea hilo amesema kitendo cha kuingizwa kesi iliyoko ICC kiliudhi kambi nzima ya Jubilee hivyo anastahiki kufuata ushauri wa kambi hiyo kujiondoa kwenye mdahalo wa mwisho kabla ya uchaguzi. Aidha, kumekuwa na tetesi kutoka kwa wanachama wa ODM, ambacho kinaongozwa na Raila Odinga, kwamba wanachama wa Jubilee wana mpango wa kuhakikisha mgombea wao Uhuru Kenyatta anashinda kiti cha urais kwa hali yoyote ile.

Suala hili limewatia wakenya tumbo joto kwani hawataki ghasia, wanaona kitendo cha wanachama wa Jubilee kung’ang’ania kupata ushindi kwa namna yoyote ile ni kutaka kuchochea ghasia miongoni mwa wakenya ambao wanataka utulivu. Wanachama wa ODM wanadai kuwa Jubilee wanataka kuiba kura ili mgombea wa Jubilee, Uhuru Kenyatta ashinde kiti hicho, jambo ambalo hawajathibitisha hadi sasa.

Hii imekuwa kashfa ya kwanza kutolewa kwenye kampeni za uchaguzi zinaoendelea hapa Kenya. Aidha, hawa ODM hawasemi ni namna gani Jubilee ya Uhuru Kenyatta watakavyoiba hizo kura, bali wanaendelea kushutumu na kuchochea matumbo moto kwa wapigakura. Chama cha Jubilee ambacho kinaongozwa na Uhuru Kenyatta na mgombea mwenza Wiliam Rutto, kimejaribu kufanya kila njia kupinga tetesi za  wanachama wa ODM wanaoongozwa na Raila Odinga kwamba walitaka kuiba kura.

Wengi wanasema haifai kwa ODM na Odinga kueneza fitina kama hii ambayo haina chembe ya ukweli. Wanasema kama Odinga hakujifunza kwa Uhuru Kenyatta na Ruto juu ya mashtaka yao kule ICC, ni vema akachunga kauli zake uchwara ambazo zinachochea uharibifu wa amani kwa wapigakura.

Kulingana na utafiti ambao umefanywa na baadhi ya kampuni nchini Kenya, Raila Odinga anamshinda Uhuru Kenyatta kwa asilimia chache sana, huku wakifuatwa na wagombea wengine. Wagombea hawa wawili wanafuatana uso kwa uso na wakenya wanatarajia mmoja wao kuibuka mshindi baada ya uchaguzi wa Machi 4, mwaka huu.

Huku uchaguzi ukikaribia, serikali iliamua kuunda Tume ya Taifa ya Uwiano na Utangamano, ikiwa na lengo  la kuwaunganisha Wakenya na kuwachukulia hatua wakali wanasiasa na wananchi wanaotoa matamshi ya kichochezi. Mwenyekiti wa tume hiyi ni Mzalendo Kibunja, ambaye amesema Tume yake haitamuonea aibu mwanasiasa na mwananchi yeyote atakayeleta uchochezi kwa wakenya. Wengi wanakumbusha ikwemo hatua ya ODM, kusema Jubilee wataiba kura, kuwa inabidi Mzalendo Kibunja achukue hatua kali zaidi dhidi yao.

Katika mahojiano na mwanahabari Jimmy Gathu wa kituo cha Citizen hapa Kenya, Mzalendo Kibunja, alisema kuwa wale wote wanaoeneza matamshi ya kichochezi na chuki watachukuliwa hatua kali.

Hatua ya tume ya Uwiano na utangamano, imekwenda mbali zaidi na imewaonya wanaotumia mtandao wa facebook na Twitter kuwa makini kwa maandishi yao wanayowaeleza wenzao kuhusu uchaguzi mkuu wa hapa Kenya.

 Uhuru Kenyatta

Jaji mkuu wa Kenya Dk. Willy Mutunga ametangaza kuwa anatishwa na baadhi ya wanasiasa, hali ambayo inamfanya asiwe na amani na kukisia kuwa huenda uchaguzi huu unaweza kuwa na machafuko pia. Jaji Mutunga anadai kuwa vitisho hivi vinamshinikiza kutekeleza maslahi yao badala ya kujali uamuzi wa wakenya kwenye uchaguzi.

Hata hivyo, Jaji huyo alisema kwamba vitisho dhidi ya Idara ya Mahakama havitawafanya majaji kutekeleza maslahi ya kundi fulani la watu. Jaji alisema kwamba alipokea vitisho hivi karibuni wakati wa kesi iliyowahusisha Uhuru Kenyatta na William Rutto ilipokuwa ikisikilizwa huko nchini Uholanzi. 

Alieleza jinsi ujumbe wa barua aliyoipokea ilivyokuwa ikimtisha, na kwamba angetendewa jambo baya na kundi haramu la Mungiki, iwapo angetoa uamuzi wasioupendelea katika kesi ya wawili hao. 

Mwaka wa 2007, ilisemekana kwamba Uhuru  Kenyatta alitumia kundi hili kuwaangamiza Wakalenjin Mkoani Rift Valley. Jaji Mutunga analaumu serikali kwa kumdhulumu baada ya kuamrishwa na afisa mmoja wa uhamaji, kusafiri kwenda Dar es Salaam kwani hakuwa na idhini ya mkuu wa Umma, Francis Kimemia.

Jaji mkuu ameeleza hofu yake ya majaji kutishwa kisiasa huku uchaguzi ukikaribia kwani inahatarisha usalama wao na kuiweka nchi kwenye hatari ya machafuko. Jaji huyo alitangaza msimamo wake kuwa hatatishika na kama mmoja wa wapiganaji wa demokrasia, yuko tayari kwa lolote.

Jambo jingine ambalo linafanyika katika uchaguzi huu ni matayarisho ya karatasi za kupigia kura yanayofanywa na Tume Huru ya Uchaguzi (IEBC). Pia IEBC imeamua kuachana na majaribio ya uchaguzi yaliyopangwa kufanyika mapema Februari 24. 

Katibu wa IEBC, James Oswago alisema kuna kazi ngumu kufanya majaribio badala ya uchaguzi kamili. Hivyo mashauriano yalifanyika kwamba majaribio yafanyike Februari 18 yaani Jumatatu iliyopita ili kuwaruhusu wananchi kupigakura kwa ufasaha ifikapo Machi 4.

Naye meneja wa Elimu kwa wapigakura IEBC, Nixon Ng’ang’a alisema kwa mara ya kwanza katika historia ya hapa Kenya, wapigakura watakuwa wanpiga kura kwa nafasi za uchaguzi sita na siyo tatu, hivyo watahakikisha zoezi linakwenda vema. Kwingineko ni shamrashamra zinazoendelea hapa, kwani IEBC imesema wagombea wote nane wanatakiwa kufanya kampeni za amani ili kuwalinda wakenya dhidi ya machafuko.

Dorine Otinga ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Egerton nchini Kenya na atakuwa miongoni mwa wasimamizi wa uchaguzi huo.

No comments:

Post a Comment