Pages

Pages

Tuesday, March 12, 2013

Mkutano wa dharula Simba upo mikononi mwa Rage



Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MKUTANO wa dharula unaohitajiwa na wanachama wa Simba, upo mikononi mwa mwenyekiti wake, Ismail Aden Rage, aliyekuwa nje ya nchi, licha ya baadhi ya watu kuhitaji mkutano huo kwa ajili ya kujadili mambo ya klabu yao.


Mapema wiki iliyopita, katika ziara yake kwenye tawi maarufu la Mpira Pesa kwa ajili ya kuvunja makundi, Mwenyekiti wa Kamati ya Ushindi, Rahma Al- Kharoos, aliambiwa kuwa ili wanachama wa Simba watulie, lazima wakubali kuitisha mkutano unaopigiwa kelele.

Mwenyekiti wa tawi hilo, Ustadh Masood, alisema kuwa bila kufanya mkutano huo hawawezi kuacha harakati zao za kuikomboa klabu yao, ambayo kwa sasa tayari imeshaingiwa na mdudu mbaya wa viongozi wao kujiuzulu.

Alisema kuwa hata ziara ya Malkia wa Nyuki kwenye tawi lao, ingawa lilikuwa na mashiko kwa ajili ya kudumisha ushirikiano wao, lakini wanachama wa Simba lengo lao ni mkutano kwa ajili ya kuijadili timu yao ambayo imeshapoteza nafasi ya kutetea taji lao.

“Sisi hatuna lengo la kuihujumu timu yetu, ndio maana tulichokuwa tunapigania kimeonekana baada ya Simba kukosa nafasi ya kutetea ubingwa wake, pamoja na kutolewa kwa aibu ligi ya Mabingwa Afrika, dhidi ya Libolo.

“Tulimwambia Malkia wa Nyuki kuwa kama lengo ni kuifanya timu iwe moja, basi ahakikishe viongozi wenzake wanaitisha mkutano kabla ligi haijakwenda mwisho, ukizingatia kwamba kwa sasa mambo yamekuwa magumu mno,” alisema.

Naye Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema kuwa kwa sasa mkutano huo hauwezi kujadiliwa hadi mwenyekiti wao, Rage, arudi kutoka nje ya nchi, ukizingatia kuwa ana zaidi ya wiki mbili hayupo Tanzania.

“Tulikubaliana kwa mambo mengi, isipokuwa suala la mkutano wa dharula haliwezi kupatiwa ufumbuzi kwakuwa mwenyekiti hayupo, hivyo naamini kuwa mara baada ya kurejea, basi kitajulikana kila kitu kwa ajili ya kuifanya Simba iwe moja,” alisema Kamwaga.

Mwishoni mwa wiki, Simba ilifanikiwa kuwaridhisha mashabiki wao kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union ya Tanga, mechi iliyokuwa na ushindani wa aina yake kutokana na kila mmoja kuipania ili iibuke na ushindi.

No comments:

Post a Comment