Pages

Pages

Monday, February 18, 2013

Tatizo ni Malinzi, Wambura au Kamati za Tenga



 SIWEZI KUVUMILIA

Rais wa TFF, Leodgar Tenga kulia, akiwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Sunday Kayuni.
 
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
SIKU ya kutangaza majina ya watu waliopitishwa na Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka nchini (TFF), nilipata nafasi ya kumuuliza swali Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Deogratius Lyatto, katika ofisi hizo zilizopo Karume, Ilala, jijini Dar es Salaam.

Swali lilijikita zaidi kwenye kipengele cha uzoefu, hasa kwa kuona Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji, amepitishwa kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, hali ya kuwa hajawahi kuwa kiongozi katika soka, ukiacha udhamini wake.

Hakika, majibu yalikuwa ni siasa tupu. Eti Lyatto akajibu, una miaka mingapi kwenye uandishi wa habari za michezo? Nikamjibu nilivyoona inafaa. Naye akauliza tena, je tukitangaza nafasi za kugombea kwa sifa zako hizo utajitokeza? Namimi nikamjibu ndiyo.


Kisha akamalizia, basi hata huyo Manji ana sifa ndio maana amepitishwa. Nakumbuka sikuwa na hoija nyingine zaidi ya kuguna, nikaona hapa nimedanganywa, hivyo kuwa njia ya kwenda kuwadanganya Watanzania kutokana na udhaifu wa Kamati za TFF.

Kwanini nilikuwa na wasiwasi na suala hilo? Ukiangalia kanuni za Uchaguzi hasa kwenye bodi ya Ligi, uzoefu unatajwa kuwahi kuongoza soka au kucheza soka. Kama hata kudhamini basi una uzoefu, basi hakuna mwandishi wa habari za michezo anayeweza kuenguliwa kwenye uchaguzi huo kwasababu tayari wapo kwenye sekta ya mpira wa miguu.

Kama siyo hivyo, basi tutaongeza mkanganyiko wa aina yake. Haya yakapita, lakini nikashangaa tena pale Kamati ya Rufaa ilipomuengua Jamal Malinzi kwa kisingizio kama hicho cha uzoefu? Jamani, Malinzi aliwahi kugombea mwaka 2008 na rais anayemaliza muda wake, Leodgar Tenga na kura hazijatosha.

Kigezo gani pia kimetumika kumuengua Malinzi kwa Kamati ya Rufaa wakati kule kwenye Kamati ya Uchaguzi haijaonekana tatizo hilo? Hata hivyo haitoshi, huyu aliyemuwekea pingamizi Malinzi, anayejulikana kama Agape Fue, ni nani?

Kwanini pingamizi lake lilitupwa na Kamati ya Uchaguzi kwasababu hajakuwapo kwenye usaili au kupitia pingamizi na baadaye kusikilizwa ambapo pia majibu yalitoka na kupewa haki? Hili siwezi kuvumilia.

Na ndio hoja yangu ya leo nikiona kuwa tatizo ni Malinzi, Wambura au Kamati za Tenga? Hakika maswali kama haya yanatesa. Tanzania tumetumia muda mwingi kuendelea kujenga misingi ya kuendeleza soka letu, hivyo inashangaza kama wapo wachache wanaotaka kuturudisha huko.

Inawezekana sisi ni marafiki sana, lakini kwenye masuala muhimu kama haya, ni vyema tukatoa maamuzi kwa kuangalia Katiba inavyosema. Soka limekuwa na matatizo mengi. Kelele zimeshika kasi, hivyo hatuwezi kusonga mbele.

Kamati za Tenga, hazina mashiko tena. Maamuzi yao yamejaa ushabiki, kukomoana na sioni haki ikitendeka. Kwa mfano, juzi Tenga alipozungumza na waandishi wa habari, alisema kuwa walioenguliwa wasilalame badala yake wasubiri maamuzi ya review ya Kamati ya Rufaa baaada ya kumalizia kupitia kama walivyoombwa na Malinzi, aliyenguliwa katika nafasi ya Mgombea Urais, akibakia mgombea pekee, Athumani Nyamlani.

Tenga anasema hayo, huku akijua siku za uchaguzi zimekaribia, maana kwa mujibu wa TFF, Uchaguzi huo umepangwa kufanyika Februari 24 mwaka huu. Ina maana bado siku chache mno, hivyo kama wadau hao watasubiria kikao hicho, vipi majibu yakitoka yasiyokuwa ya kuridhisha, ni wapi, lini watapata haki yao ya msingi?

Ukiangalia suala hili, utagundua ni ubabaishaji, kudanganya na kuendelea kuweka dhana ya kulindana, ingawa tukisema hili wachache wao watapinga au watatuona tofauti. Huo sio mpango mzuri. Hatuwezi kusonga mbele kamwe.

Watendaji wetu, viongozi, wakiwamo hao wa TFF wanapaswa kujua zuri lililolindwa kwa miaka 100, linaweza kuharibika kwa siku moja tu. Kama hili lilivyotokea. Kamati za Tenga zimemvua nguo mwenyewe, akijidanganya kuwa Katiba haimruhusu kuingilia maamuzi ya Kamati zake.

Kweli? Tenga anaongea kama mjumbe au Rais wa TFF? Nafikiria huu ni wakati wa kujiangalia upya kwa faida ya soka letu. Tutamlaumu Michael Wambura bure, lakini udhaifu upo kwenye Kamati zinazofanya kazi kwa mashinikizo ya watu.

Haki hakuna, ingawa inatakiwa ionekane ikitendeka badala ya kutajwa tu kuwa inafanyika, hivyo katika hili ni aibu ya mwaka. Nadhani katika hilo, wadau wote wanapaswa kujua udhaifu huu hadi kulazimisha wengineo kukimbilia mahakama za kawaida.

Baadhi yao wanasema, soka halitakiwi kupelekwa mahakama za kawaida au serikali kuingilia kati, lakini kama watu wanakandamizwa, wanaonewa, wanabanwa, hiyo haki inayosemwa wao wataipata kwa mtindo gani?

Tunaona kabisa jinsi watu wanavyolalamika kukandamizwa, lakini hapo hapo rais wa TFF, Tenga aliyeombwa na Naibu Waziri, ambaye katika maoni hayo aliyatoa kama mdau wa michezo, anasema hawezi kuingilia.

Kwanini usiweze? Ni huko huko kulindana tu, lakini vinginevyo ningemshauri Tenga na jopo lake wajiuzulu hata kama nafasi zao zipo mwishoni. Natamani kuona Tenga anawajibika kwasababu ameshindwa kuwasimamia watu wake.

Kama hataki, basi hata kuvunja Kamati hizo kama alivyoziteuwa, ingawa leo anaona ni ngumu sana kuwa tofauti na Kamati zake, hivyo hakika udhaifu huu, kamwe hauwezi kuvumiliwa na ndio maana nimekaa na kushindwa kuvumilia.

Tusijidanganyane jamani na hakika siwezi kuvumilia.
0712 053949, 0753 806087

No comments:

Post a Comment