Pages

Pages

Saturday, February 02, 2013

Saraff: Nyota mpya katika Bongo fleva


 Aota kufanya ngoma na P Square, Jay Dee

Msanii Saraff anayeishi Marekani mwenye uraia wa Tanzania, akiwa kwenye pozi kali la kimauzo.

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KUANZIA miaka ya 2000 hadi leo, Tanzania imekuwa ikishuhudia wimbi kubwa la vijana wanaojiingiza katika tasnia ya muziki wa kizazi kipya, maarufu kama Bongo Fleva.
Saraff akiwa Studio

Tangu wakati huo pia tumeshuhudia mabadiliko makubwa katika tasnia hii, ambapo vipaji vimekuwa vikichomoza na kujipatia mafanikio ya aina yake.


Msanii Saraff akiwa kwenye pozi.

Miongoni mwa wasanii hao ni Ashraf Omar Maundi, maarufu kama Saraff, anayefanya kazi zake kwa umahiri na kuwa na malengo makubwa kisanaa.

Saraff anasema kwamba alichelewa kujitokeza katika sanaa hiyo kwa kuhofia wazazi wake, ambao alijua hawatamruhusu kufanya kazi za sanaa.

“Lakini kwa sababu kipaji hakijifichi, nikiwa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Airwing, jijini Dar es Salaam, nilianza kujishughulisha na muziki, hasa kwa kuandika mashairi na kuimba.

“Ndoto yangu ilianza kufanikiwa mwaka 2005, pale wazazi wangu walipohamia nchini Marekani nikiwa sambamba nao, ambapo nilirekodi wimbo wangu wa ‘Demu wa Kibongo’, anasema Saraff.

Msanii huyo anasema kwamba licha ya wimbo huo kutokufanya vizuri, lakini alijifunza mambo mengi yanayohusu muziki, ikiwa ni pamoja na kuingia katika darasa la masuala ya muziki.

 “Ilinibidi niingie darasani kidogo nikajifunza muziki ambapo pia niliweza kurekodi wimbo  na video. Mwaka 2010 nilitoka kwenye studio yangu kwa kutengeneza wimbo wa ‘Unanidatisha’, nilioimba kwa kuchanganya lugha ya Kiswahili na Kiingereza,” anasema.

Anasema kuwa alifarijika kuona Watanzania na wasio Watanzania nchini Marekani, wakiupokea vizuri wimbo wake, hivyo kuwa njia ya kumpatia mafanikio zaidi.

Mwishoni mwa mwaka jana, alifanikiwa kutengeneza wimbo wa kwanza kama mtayarishaji na mwimbaji, wimbo unaofahamika kwa jina la Next Flight.

“Nilikamilisha wimbo wangu, wa kwanza ambao niliuandaa mwenyewe, nitahakikisha natumia muda mwingi zaidi kuandaa nyimbo zangu mwenyewe, hii itasaidia kutoa vitu kulingana na mtazamo wangu,” anasema.

Akizungumzia soko la muziki wa Tanzania, Saraff anasema muziki unazidi kufanya vyema, ingawa safari bado ni ndefu ili kufikia kiwango cha Nigeria, Ghana na Afrika Kusini.

“Safari bado ni ndefu, wengi bado wanafanya kazi kwa kubahatisha, hivyo ni vigumu sana kuingia katika soko la kimaitafa kwa mtindo huu,” anasema.

Msanii huyo anasema kuwa yupo katika harakati za mwisho za kumalizia wimbo wake mpya wa lugha ya Kiswahili, ambao anaamini utafanya vizuri.

“Lakini pia katika kuboresha kazi zangu nina ndoto ya kuja kufanya kazi na Lady Jay Dee kwa hapa nyumbani na kwa nje P Square, natamani sana na naamini itawezekana.

“Kikubwa ninachopenda kuwaambia wasanii wenzangu ni kuhakikisha tunazidi kuboresha kazi zetu ili zifanye vizuri ndani na nje ya nchi na kwa kufanya hivyo, tutazidi kuwa na mashabiki wengi zaidi,” anasema.

Kwa sasa Saraff pamoja na kujishughulisha na masuala ya muziki, yuko mbioni kumalizia shahada yake ya kwanza katika Chuo cha York College, jijini New York, nchini Marekani.

WASIFU:
Jina: Ashraff Omar Maundi
AKA: Saraff
Alizaliwa: Januari 26 mwaka 1988.
Utaifa: Mtanzania
Umri: 25
Fani: Muziki wa Bongo fleva
Anapoishi: Jimbo la Brooklyn jijini New York, Marekani

No comments:

Post a Comment