Stars isiwang’ang’anie Samatta na Ulimwengu
Mbwana Samatta, akiwa uwanjani.
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MWISHONI mwa wiki, Shirikisho la Soka
nchini (TFF), lilitangaza kumtuma Mkurugenzi wao wa michezo, Sunday Kayuni,
kwenda nchini Kongo katika klabu ya TP Mazembe kwa ajili ya kufanya mazungumzo
juu ya wachezaji wa Tanzania wanaokipiga hapo, Mbwana Samatta na mwenzake
Thomas Ulimwengu.
Pamoja na mambo mengine, Kayuni alitarajiwa
kukutana na uongozi wa TP Mazembe ili kujadili namna gani inaweza kuwaachia
nyota hao kwa ajili ya kuitumikia timu yao ya Taifa, Taifa Stars.
Safari ya Kayuni inatokana na wachezaji hao
kuingia kwenye utata mara kwa mara wa kuachiwa na timu yao hiyo kwa ajili ya
kujiunga na kambi ya Stars, huku mara ya mwisho vijana hao hawakucheza mechi
kwasababu ya kuumwa kama walivyosema.
Kwa bahati mbaya, matokeo hayo yalikuwa
magumu sana kwao, hasa pale walipoonekana wasaliti kwa Watanzania na kujikuta
wakizomewa uwanjani, ingawa walikuwa nje ya uwanja.
Hii ni hatari, hasa kwa
kuiangalia TFF hii ambayo macho yao yote yapo kwa Samatta na Ulimwengu. Kwa
sababu hiyo, hakika siwezi kuvumilia.
TFF na wadau wengine wa soka wanapaswa
kuwekeza zaidi kwa wachezaji vijana, maana ndio suluhisho pekee la kukuza mpira
wa miguu na sio kila mmoja kuwaangalia Samatta na Ulimwengu.
Bado ni
vijana wadogo wanahitajika ndio kwenye soka, lakini kama tukiwa na wachezaji
wengine wenye uwezo kama wao, maendeleo yatakuwapo.
Najua wapo wachezaji mfano wao wanahitaji
kuitwa katika timu hiyo, lakini jinsi ya kuonekana ndio utata.
Vijana
walionea katika kila kijiji, Kata, wilaya na Mkoa hawajui namna ya kujionyesha
na kuitwa Stars. Kwa sababu hiyo, kocha Mkuu wa Stars, Kim Poulsen, anapaswa
pia aitumie vyema falsafa ya kukuza soka la vijana.
Wao ndio
nguzo na hakika hilo linajulikana kwa kiasi kikubwa. Huu ndio ukweli wa mambo.
Tanzania
imekuwa ikifanya mambo kisiasa zaidi, hata katika soka uwanjani. Hii leo kutaka
kuwang’ang’ania Samatta na Ulimwengu ni kutaka tu ajenda hiyo kuzungumzwa na
wadau wa michezo. Tayari wachezaji hao wamesharipo kambini kwa ajili ya kujiandaa dhidi ya Ethiopia.
Hatuwezi
kwenda hivyo. TFF iweke mipango zaidi kwa kuhakikisha kocha wao anatembelea
katika mikoa au wilaya zinazoshirikisha ligi za vijana zenye ushindani kutokana
na vijana wake kupania kuonyesha vipaji vyao.
Nimekuwa nikiangalia juhudi na utendaji kazi
wa viongozi wengi kwenye medani ya soka, nimegundua kuwa waliokuwa wengi,
wanaangalia zaidi wachezaji wenye majina kwa ajili ya kubeba kwenye vyombo vya
habari.
Mtindo
huu sio mzuri na ndio maana kocha wa zamani wa Taifa Stars, Mbrazil, Marcio
Maximo alilipinga kwa nguvu zote.
Kupinga kwake kulisababisha maendeleo hasa
kwa kuwapika wachezaji kama vile Samatta, Mrisho Ngassa na wengineo ambao leo
hii wamekuwa na faida kubwa katika medani ya soka.
Wadau
ambao walikuwa wakimpinga Ngassa, Kigi Makasy na wenzake leo hii ndio macho yao
na huwataja sana wasipokuwa uwanjani.
Kwa bahati mbaya, tunahitaji kuwa na vijana
wanaocheza soka la kulipwa nje yaa nchi. Lakini, kuna taratibu za wachezaji
kurudi kwenye Mataifa yao kwa ajili ya timu ya Taifa.
Sisi
kwetu Tanzania tumekuwa tukiwahitaji hata pale ambapo si wakati muafaka kwao.
Kwa timu zinazojiendesha kwa mipango hatuwezi kuelewana nao.
Labda kwa Simba na Yanga ambao mara kadhaa
wao wamekuwa watu wa sifa, wakijivunia nyota wao kuitwa Stars hata kama
wanaathiri program za kocha wao, jambo ambalo si sahihi hata kidogo.
Kulisema
hili hakuhitaji wote tuwe na digrii, maana ni dhahiri mikakati hii inaonekana
na jinsi inavyoleta usumbufu kwa kiasi kikubwa.
Ndio maana nasema siwezi kuvumilia. Tufanye
mambo yetu kwa kuangalia namna ya kutuwezesha kusonga mbele na sio kubakia
kulalama juu ya wanasoka waliokuwapo nje, akiwamo Samatta na mwenzake badala
yake tubuni namna ya kuwaongeza wengine.
0712
053949
0753
806087
No comments:
Post a Comment