Pages

Pages

Wednesday, January 02, 2013

'Sajuki alisema hawezi kuishi tena duniani'



Wastara akiwa amefunikwa uso huku akilia kwa uchungu

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NI dhahiri kuwa wakati mwingine baadhi ya watu hutabiri vifo vyao, kiasi hata ha kuwazuia ndugu zao waache kufuja fedha katika kuuguza kutokana na maradhi yao.
 Rais wa TAFF, Simon Mwakifambwa, akitangaza kamati za kuratibu msiba wa Sajuki, nyumbani kwake Tabata Bima leo.

Hii hutokea sana katikaa jamii. Baadhi yao hufikia kusema “Nasikitika siwezi tena kuishi katika Dunia hii. Mwisho wa maisha yangu"

Nimelazimika kuandika maneno haya, maana kauli ya mwisho ya msanii wa filamu, Juma Kilowoko, maarufu kama Sajuki ilikuwa ni kumtaka mke wake amuombee msamaha kwa watu wote aliowahi kuwakosea katika kipindi cha maisha yake.

Maneno haya yalikuwa mahungu kwa mwanadada Wastara Juma, mke wa marehemu Sajuki. Naomba uwaambie ndugu zangu kuwa uhai wangu tena ni mdogo sana.

Siwezi kuishi, maana sioni dalili nzuri za kuniponya” maneno haya yalitoka katika kinywa ha Wastara ambaye kwa kipindi hicho, alikuwa akilia na kusaga meno kuonyesha huzuni yake.

Jamani mimi nitaweza kuishi peke yangu? Sajuki wangu kwanini umenitendea hivyo? Yani kweli unasema nikuagie kwa watu kama hutapona kumbe kweli umeshajua unaniacha peke yangu,” Wastara aliendelea kulalama, huku akizidi kufunikwa uso wake.

Inauma sana. Sajuki amekufa katika kipindi ambacho watu wengi walifahamu uhai wake utaendelea kuwapo. Kama Sajuki alistahili kufa, basi ingekuwa mwaka jana alipokuwa kwenye hali mbaya kiasi cha kulazimika kuchangiwa na wasamalia wema kwa ajili ya kwenda India.

Kwa mujibu wa taarifa, Sajuki alipokwenda India, maradhi yaliyompeleka ya Tumbo yaliongezeka mengine ya Kansa ya ngozi. Shughuli ilikuwa kubwa sana. Mbaya zaidi, Sajuki hakuwa na uwezo wa kustahimili ugonjwa wake.

Hata hivyo, katika kipindi cha mwisho wa mwaka 2012, Sajuki alikuwa kwenye afya kiasi Fulani. Muda wote alikuwa akisikika akimshukuru Mungu wake kwa kumpa uhai.

Katika kumshukuru Mungu, Sajuki pia alikuwa haishi kumshukuru Mungu kwa kumpa mke mwema, mwenye upendo wa kweli. Mwanamke ambaye licha ya kukutana na vikwazo vingi, lakini aliendelea kufunga khanga yake akitetea upendo wake kwa Sajuki.

Kwanini? Pamoja na yote hayo, lakini leo tunaongelea kifo chake. Na saa tano za asubuhi, keshokutwa Ijumaa, mwili wake utazikwa katika makaburi ya Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Msiba wake ni mzito sana. Wasanii wote pamoja na wadau wanalia. Serikali nayo kwa kupitia Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo inalia kutokana na msiba wa Sajuki.

Amekufa na katika kipindi ambacho watu wanashangaa kwanini bundi wa vifo vya wasanii wa maigizo na filamu anaendelea kukaa kwenye paa za nyumba za wasanii hao Tanzania?

Sajuki amekufa katika kipindi cha siku 37 kabla ya arobaini ya msanii Hussein Mkiety, maarufu kama Sharomillionea, inayotarajiwa kusomwa Januari nne, kijijini kwao Lusanga.

Mamia ya watu walikuwa wakimiminika katika viwanja vilivyokuwapo nyumba ya marehemu Sajuki, maeneo ya Tabata Bima. Ukifika hapo nyuso zao zinasema.
Wengi wanalia na kuomboleza kifo hicho. Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), kwa kupitia Rais wake, Simon Mwakifambwa na wadau wengine wamekuwa wakipita huku na kule kwa ajili ya kuweka sawa taratibu za msiba huo wa Sajuki.
Taarifa ya Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangara amewatumia salamu za rambirambi, ndugu, jamaa na wasanii wote nchini kufuatia kifo cha Sajuki ilimuumiza na kutaka Watanzania kumuombea dua njema.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo kifo chake ni pengo kubwa kwa Serikali, wadau wa tasnia ya filamu na michezo ya kuigiza nchini kwa ujumla. “Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Sajuki na sina maneno ya kuelezea masikitiko na huzuni nilinayo, kwani kifo chake ni pigo katika tasnia ya filamu za michezo ya kuigiza,” alisema Dkt. Mukangara.

Dkt. Mukungara amewataka ndugu, jamii na wasanii wote kuwa wavumilivu na watumilivu wakati wote wa msiba na kumuombea marehemu makao mema kwa Mwenyezi Mungu. Sajuki ni mzaliwa wa mkoa wa Ruvuma na sanaa yake alianza kujihusisha nayo alipojiunga na kikundi cha Kaole Sanaa Group, ambapo baadaye alicheza filamu Revenge  ya Kampuni ya RJ.

Mwaka 2008 aliamua kuanza kutengeneza kazi zake mwenyewe ambapo filamu yake ya kwanza iitwayo Two Brothers  kwa kushirikiana na Shija  Deogratious ilitoka. Sajuki baadaye aliamua kuanzisha kampuni yake iitwayo WAJEY Production Company ambapo alitengeneza filamu nyingi zikiwemo Mboni Yangu, Round, Briefcase , Kijacho, Kozopata, Mchanga na Keni, 077( Zero Seven Seven).nk 


Sajuki alifanikiwa kucheza michezo ya kuigiza na filamu na wasanii wengi wenye majina hapa nchini. Sajuki amebobea katika Uigizaji, Utayarishaji na Uongozaji wa filamu. Sajuki alianza kuugua mwaka 2010 na hali ilizidi kudhoofu mwaka 2011, ambapo alikwenda kutibiwa nchini India kutokana na michango kutoka kwa wadau tasnia ya filamu. 

Alirudi na kuonekana kapata nafuu kidogo jambo ambalo lilileta matumaini na furaha kwa watanzania; aliporejea tu aliweza kutoa filamu iitwayo Kivuli  huku filamu nyingine ikiwa katika hatua ya utengenezaji.

Ambapo pia filamu ya kumchangia iliandaliwa na kuitwa Sayla na kushirikisha wasanii na viongozi wa serikali, akiwamo Zitto Kabwe, ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, January Makamba na wengineo.

No comments:

Post a Comment