Mbunge wa Kinondoni, Idd Azan.
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MBUNGE wa Kinondoni kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),
Idd Azan, amepangwa kuwa mgeni rasmi katika pambano la Ubingwa wa Taifa,
litakalowakutanisha Japhet Kaseba na Ramadhan Maneno, liliopangwa kufanyika
Machi 2 mwaka huu, katika Ukumbi wa DDC Magomeni Kondoa, jijini Dar es Salaam.
Pambano hilo ndilo linalosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa
masumbwi, likiwakutanisha wakali wa ndondi, akiwamo Kaseba, aliyewahi kuwika
pia kwenye ngumi za mateke.
Akizungumza na Handeni Kwetu, Kaseba alisema kuwa pambano lao litahudhuriwa na mbunge wa Kinondoni, akiwa na
shauku ya kutaka kujua nani mkali.
Alisema katika masumbwi hayo, kila mmoja anataka kuonyesha
makali yake, huku yeye akiwa na hamu zaidi ya kuonyesha kwanini anakimbiwa na
mabondia wengi.
“Nimekuwa nikikimbiwa sana na mabondia hapa nchini, hivyo
naamini katika pambano hili ambalo mgeni rasmi atakuwa mbunge wa Kinondoni,
nitaonyesha ukweli huo.
“Kila kitu kinaendelea vizuri kuelekea katika patashika hiyo
itakayokutanisha pia mabondia wengine wenye uwezo, akiwamo Mtambo wa Gongo na
wengineo,” alisema.
Mwaka jana Kaseba alishindwa kupigana na Francis Cheka,
licha ya kutangazwa mno na wadau wa ngumi na kupangwa kufanyika katika Ukumbi
wa Dar Live, Mbagala.
No comments:
Post a Comment