Hifadhi ya Taifa ya Serengeti imeteuliwa kuwa mshindi wa Tuzo ya Kimataifa ya Utalii, Hoteli na Huduma za Vyakula kwa mwaka 2013. Uteuzi huu umefanywa na kamati ya uteuzi ya tuzo hizo baada ya Serengeti kukidhi vigezo vilivyowekwa na waandaaji wa tuzo hizo.
Taarifa iliyotumwa na Meneja Uhusiano wa Hifadhi za
Taifa Tanzania, Paschal Shelutete ilisema kuwa Shirika la Hifadhi za Taifa
(TANAPA) litapokea tuzo hiyo itakayotolewa kwa Serengeti katika hafla maalum itakayofanyika
mjini Madrid nchini Hispania tarehe 30.01.2013. Tuzo hizi huandaliwa na taasisi
maarufu duniani inayofahamika kama Global Trade Leaders’ Clubinayohusisha
makampuni yapatayo 7000 duniani.
Tuzo hii
ilianzishwa kwa ajili ya kutambua na kuenzi michango inayotolewa na taasisi na
makampuni yanayojihusisha na utalii, hoteli pamoja na huduma za vyakula kama
njia ya kuthamini mchango na kuhamasisha wale wote wanaofanya kazi katika sekta
hii ambayo ni muhimu katika maendeleo ya uchumi wa nchi husika.
Hafla ya
utoaji wa tuzo za mwaka huu itahudhuriwa na wadau wa shughuli za utalii kutoka
nchi zipatazo 40 duniani na zitaambatana na Maonyesho ya Kimataifa ya Utalii
yanayofanyika kila mwaka mjini Madrid, maarufu kama FITUR ambayo
Tanzania ni mshiriki.
Hifadhi ya
Serengeti ni hifadhi kongwe nchini ambayo ilianzishwa miaka zaidi ya hamsini
iliyopita na ambayo pia ni Eneo la Urithi wa Dunia. Hifadhi hii ni maarufu kwa
Nyumbu wahamao kila mwaka katika mzunguko unaohusisha nchi mbili za Tanzania na
Kenya. Mzunguko huu wa wanyama wahamao unaaminika kuwa ndio pekee uliobakia
ulimwenguni unaohusisha wanyama wakubwa wa ardhini.
Kutolewa kwa
tuzo hii ambayo ni heshima kwa TANAPA na nchi kwa ujumla ni matokeo ya sera
nzuri za uhifadhi zinazosimamiwa na TANAPA katika kuhakikisha kuwa maeneo
yaliyotengwa kisheria kama Hifadhi za Taifa yanaendelea kuhifadhiwa vema kwa
ajili ya vizazi vijavyo lakini pia kuhakikisha kuwa viwango vya huduma za
utalii katika hifadhi zinakuwa za kiwango cha kimataifa ili kuhudumia wageni
watokao sehemu mbalimbali ulimwenguni.
No comments:
Post a Comment