Pages

Pages

Wednesday, January 02, 2013

DC Kilindi anusuru machafuko ya wakulima na wafugaji


Mkuu wa Wilaya Kilindi, Selemani Liwowa

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MKUU wa Wilaya ya Kilindi, mkoani Tanga, Selemani Liwowa, amenusuru kutokea kwa machafuko ya wakulima na wafugaji katika wilaya yake, baada ya wakulima wa kijiji cha Mswaki kuwateka ng’ombe waliokuwa kwenye mashamba yao na kuwapeleka kijijini kama ishara ya kuonyesha uharibifu unaofanywa na wafugaji katika vijiji vyao.

Hatua hiyo ilisababisha kutoelewana na kumfanya Mkuu wa wilaya kwenda katika kijiji hicho wiki iliyopita kwa ajili ya kuangalia tatizo na kuepusha mgogoro huo unaosumbua katika vijiji vya wilaya Kilindi na Tanzania kwa ujumla.

Akizungumza na Handeni Kwetu, kwa njia ya simu, DC Liwowa alisema kwa uchunguzi wao umegundua kuwa baadhi ya wenyeviti wa vijiji vyao wanaruhusu kuingia kwa wafugaji bila kufuata utaraatibu jambo lililoleta balaa katika kijiji cha Mswaki na Turiani, wilayani kwake.

Alisema wakulima hao waliamua kuwachukua ng’ombe hao naa kuwapeleka kijijini kwa ajili ya kushitaki kwa serikali ya kijiji, lakini baadaye wafugaji hao walibadilisha na kusema kuwa mifugo yao imetekwa kwa ajili ya kuiba.

“Hili ni tatizo lililotokea wiki iliyopita na wala sio jipya kama inavyodaiwa, hasa baada ya wafugaji wanaoachia ng’ombe zao kulalama kwa kusema kuwa mifugo yao imetekwa na wakulima, hivyo kuleta kutoelewana miongoni mwao.

“Mimi na ujumbe wangu tulipata fursa ya kwenda katika maeneo yale kuweka mambo sawa, hivyo tuligundua kuwa baadhi ya wenyeviti wanaruhusu wafugaji kuendelea kuingia katika sehemu zao bila kuangalia athari zinazoweza kujitokeza,” alisema.

Migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji imeendelea kuwa tatizo katika wilaya mbalimbali hapa nchini, jambo linalotakiwa liangaliwe upya na Watanzania wote, wakiwamo viongozi wa vijiji, Kata, Tarafa na wilaya kwa ujumla.


No comments:

Post a Comment