Pages

Pages

Sunday, December 30, 2012

Vifo 5 vya wasanii vilivyotikisa Tanzania 2012



Marehemu Steven Kanumba

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
HII ni Jumamosi ya mwisho kabla ya mwaka huu kumalizika na kuuanza mwaka mpya wa 2013. Ni mwaka uliokuwa na matukio mengi katika sekta karibia zote.
Sharomillionea kabla ya umauti wake
 
Sio kisiasa, kimichezo na kiutamaduni. Pande zote hizo zimeguswa na matukio ambayo kwa kiasi Fulani yaliumiza watu na kuwaacha njia panda kwa kiasi kikubwa.

Hapa nitaelezea japo kwa ufupi matukio ya kisanaa na burudani hasa ya vifo yaliyotokea kwa mwaka huu, ambayo kwa kiasi kikubwa yalitikisa katika viunga hivyo nchini.

 Mariam Khamis, enzi za uhai wake

Yalichanganya kiasi kwamba hadi sasa, ukimuuliza mtu anayefuatilia sanaa nini anakumbuka kwa mwaka huu, ni wazi atakwambia misiba isiyopungua mitano ya wasanii wetu.

Misiba ambayo imeacha pengo kubwa. Watu bado wanaendelea kulia na kuumizwa na misiba hiyo. Tena misiba mingine mitatu imetokea ndani ya kipindi cha mwezi mmoja ule wa Novemba.

Tuanze na msiba wa kwanza uliogusa watu wengi na kulifanya jiji zima litetemeke. Kila mdau wa sanaa aliumia. Si mwingine, bali ni msiba wa Steven Kanumba, uliyotokea nyumbani kwake Sinza Vatcan, jijini Dar es Salaam, Aprili 7.

Kifo cha msanii huyo wa filamu hapa nchini kilihuzunisha wengi. Siku ya Aprili 8, takribani vyombo vya habari vyote viliripoti msiba huo na kufanyia mwendelezo katika kipindi cha zaidi ya siku 30.

Msiba huo inadaiwa ulitokana na ugomvi wa kimapenzi kati yake na msanii mwenzake Elizabeth Michael, maarufu kama (Lulu), ambaye hadi leo yupo rumande.

Mwili wa Kanumba uliagwa katika viwanja vya Leaders Club, kabla ya kuzikwa makaburi ya Kinondoni, huku msiba wake ukivunja rekodi kutokana na kujaza watu wengi.

Jiji zima lilifurika watu. Tax zilifanya kazi pamoja na bodaboda zilizobeba watu kuwatoa sehemu moja kwenda nyingine, hasa wale waliokuwa na haraka ya kufika eneo la tukio.

Kwa mwaka huu, msiba wa Kanumba ndiyo uliyokusanya watu wengi kwa mara moja, hasa kutokana na umahiri wake katika kazi, akicheza filamu nyingi zinazopendwa hadi leo.

Kanumba tayari alishaanza kuvuka nje ya mipaka ya Tanzania kwa kucheza filamu zaidi ya tatu za Kimataifa, ikiwamo ile ya Dar to Lagos.

Baada ya msiba huo kupoa na watu kuendelea na maisha ya kawaida, mwishoni kabisa mwa mwaka huu, msiba mwingine ulitokea katika tasnia ya taarabu, Mariam Khamis kupoteza maisha.

Mwanadada huyo aliyekuwa anafanya kazi na TOT Taarab, chini ya Malkia wa Mipasho Tanzania, Khadija Omari Kopa, alifariki kutokana na matatizo ya uzazi na kuacha kichanga.

Mwanadada huyu alizikwa katika makaburi ya Magomeni Ndugumbi, ikiwa ni siku moja tu baada ya kifo chake. Kutokana na imani ya dini yake ya Uislamu, mwimbaji huyo alizikwa mapema.

Msiba wa Mariam uligusa watu wengi katika tasnia hiyo ya taarabu, wakijitokeza watu wengi wa kushiriki mazishi yake. Hata hivyo, bado hajaweza kufikia hata robo ya watu waliomzika marehemu Kanumba.

Msiba wa Mariam Khamis ulikuwa mzito kwa wadau wa taarabu hapa nchini, ukizingatia kuwa alikuwa na mashabiki waliopenda kazi zake alipokuwa kwenye kundi hilo linalomilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Wakati watu wanaendelea kutafakari maisha ya sanaa na wasanii hapa nchini, wadau walishtushwa na taarifa za msiba wa msanii wa zamani wa Kaole, Khalidi Mohamed, maarufu kama Mlopelo, kilichotokea Novemba 23.

Msiba wa msanii haujatingisha sana, labda ni kwasababu hakucheza nafasi zinazokaa kwenye fikra za watu kichwani au maisha ya Kaole Sanaa Group yalivyokuwa yakishuka kwa kasi.

Ilikuwa hadi mtu amuelezee sana ndio mtu akumbuke sura yake au kumuona kwenye picha yake. Hata hivyo pengo lipo, maana kila mtu ana umuhimu wake katika jamii.

Msiba wa Mlopelo bado ukiwa mbichi, taarifa za kifo cha John Maganga nazo zilisikika na kuzidi kuwaacha watu kwenye maswali mengi wakiangalia namna gani habari hizo zinakuwa nyingi kwa wasanii.

Taarifa za kifo cha Maganga zilichanganya watu wengi, tangu Novemba 25, wakipishana siku moja, ukingatia kuwa msiba huo ingawa haujafikia mshtuko wa Kanumba, ila wengi walimjua na kuheshimu kazi zake za sanaa hapa nchini.

Moja ya kazi aliyocheza marehemu Maganga ni ile ya Mrembo Kikojozi iliyofanya vyema katika tasnia hiyo ya filamu Tanzania.

Maganga alizikwa makaburi ya Kinondoni, lakini siku aliyokuwa anazikwa, mwingine ulitokea, huu ukiwa mkubwa zaidi kwa wasanii na wadau wa sanaa kwa ujumla.

Msiba huu ulikuwa ni wa Hussein Mkiety, maarufu kama Sharomillionea, uliyotokea Novemba 27 mwaka huu. Kijana aliyeibadilisha kabisa soko la sanaa ya vichekesho. Wengi walizoea kuigiza wamevaa vinyago.

Lakini ujio wake ukawa na matunda zaidi. Mwonekano wake wa usafi zaidi, lakini bado alichekesha. Ni kazi nzuri. Marehemu Sharomillionea alikufa kwa ajali ya gari wilayani Muheza na kuzikwa katika makaburi ya kijiji chao cha Lusanga, wilayani humo.

Ukitaka kupanga misiba iliyogusa hisia za wengi, basi huu wa Kanumba ulishika nafasi ya kwanza na Sharomillionea akishika namba mbili, ingawa utaratibu huu ni mchungu zaidi, maana kiubinadamu huwezi kufananisha kupendeza kwa misiba.

Handeni Kwetu ilikuwapo katika mazishi ya msanii huyo wa vichekesho aliyeliza wengi mkoani Tanga na Tanzania kwa ujumla, huku umati wa watu ukifunga katika mtaa mzima nyumbani kwa Sharomillionea.

Pamoja na vifo vya wasanii hao, kazi zao, uwezo wao utaendelea kukumbukwa na wengi, huku kazi iliyobakia ni kuwaombea kwa Mungu ili wakapumzike kwa amani.

0712 053949
0753 806087

No comments:

Post a Comment