Pages

Pages

Wednesday, December 05, 2012

Tenga ajitetea mabadiliko ya Katiba TFF

Rais wa TFF, Leodgra Tenga.

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amesema hakuna hila yoyote katika nia ya kutaka marekebisho matatu kwenye katiba kabla ya uchaguzi na kuwataka wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF kuridhia mabadiliko hayo kwa maslahi ya maendeleo ya mchezo huo.
 
Tenga alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kufafanua juu ya waraka wa kuomba ridhaa ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF kuridhia mapendekezo matatu ya mabadiliko ya katiba yanayohusu uingizaji wa kipengele cha utoaji leseni kwa klabu (Club Licensing); kuundwa kwa Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi wa TFF na kuondoa nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais wa TFF.
 
Hatua ya kutuma waraka wa kuomba ridhaa ya mabadiliko hayo imetafsiriwa tofauti na baadhi ya wadau, wengine wakisema ni mbinu za uongozi wa sasa kutaka uendelee kukaa madarakani wakati wengine wakitaka ufafanuzi wa vipengele hivyo.
 
“Hakuna hila hata kidogo. Yote ni mambo ya maendeleo na nia yetu ni kufanikisha ili mambo yaendelee,” alisema Rais Tenga kwenye ukumbi wa mikutano wa TFF.
 
“Tusifikie sehemu tukaanza kulaumu kwa nini mtu ametaka maelezo. Lakini sikutarajia kuwa mtu wa mpira akiambiwa hili ni agizo la FIFA (Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu), atasita; akiambiwa hili ni agizo la CAF (Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika), atasita, au akaambiwa huu ni uamuzi wenu wenyewe, akasita.”
 
Tenga alisema nia ya Kamati ya Utendaji ya TFF ilikuwa ni kuitisha Mkutano Mkuu kwa ajili ya mabadiliko hayo ya katiba, lakini akasema
baada ya kutafakari kwa kina na kuangaliwa uwezo wa Shirikisho, Kamati iliona haiwezi kuitisha mikutano miwili kwa sasa kwa kuwa TFF haina fedha.
 
“Tumetoa maelezo kuwa tunafahamu kuwa katika mazingira ya kawaida tungeitisha mkutano mkuu; tuje tuzungumze na baadaye siku ya pili watu waondoke halafu tuwaite tena kwa ajili ya mkutano wa uchaguzi,” alisema Tenga ambaye alibainisha kuwa gharama za chini za mkutano mkuu wa TFF ni kati ya sh. milioni 90 na sh. milioni 110.
 
“Lakini tumeeleza bayana kuwa uwezo huo hatuna, tungelikuwa nao wala tusingefika mahali hapa; vijana wetu wanahangaika hadi tunatafuta watu watusaidie. Kwa hiyo tukasema kuna dhambi gani kuwa wakweli. Katiba inasema mkitaka kufanya mabadiliko ya katiba, itisheni mkutano mkuu. Unaita Mkutano Mkuu kwa sababu gani, ili mlete wajumbe wa mkutano mkuu ambao ndio watakaopitisha mabadiliko hayo na ndio maana tumeona dhana hiyo ya kutuma waraka.”
 
Kuhusu mabadiliko hayo, Tenga alifafanua kuwa maagizo kuhusu utoaji leseni kwa klabu (Club Licensing) na kuundwa kwa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi wa TFF yalitolewa mwishoni Julai, ikiwa ni baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji cha Julai na hivyo suala hilo kulazimika kuzungumzwa kwenye kikao cha Septemba.
 
Alisema: ”Pamoja na kwamba Tanzania ilishaingiza kwenye kanuni za ligi masharti ya utoaji leseni, CAF imekuja na maagizo kwamba ni lazima itamkwe kwenye katiba kuwa TFF itatoa leseni kwa klabu kwa mujibu wa maagizo ya CAF na msipofanya hivyo klabu zenu hazitaruhusiwa kushiriki mashindano ya klabu ya Afrika mwakani,”
 
Simba na Azam FC zitaiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya Klabu Bingwa ya Afrika na Kombe la Shirikisho, hivyo kutopitishwa kwa mabadiliko hayo mapema kutasababisha wawakilishi wa Tanzania wazuiwe kushiriki michuano hiyo.
 
Kuhusu kuundwa kwa Kamati ya Rufani, Tenga alisema baada ya kuomba ufafanuzi wa utata uliojitokeza katika vyombo vya maamuzi vya TFF, FIFA ilisema ili kuondoa mgongano wa kimaslahi, ni muhimu ikaundwa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi wa TFF badala ya mfumo wa sasa ambao Kamati ya Rufani hujigeuza kuwa Kamati ya Rufani za Uchaguzi inapofikia wakati wa uchaguzi mkuu wa TFF.
 
“Kwa hiyo tunachoomba hapa ni ridhaa ya wajumbe wa Mkutano Mkuu kwamba iwepo Kamati ya Rufani ya Uchaguzi wa TFF ili kama mtu hatatendewa haki na Kamati ya Uchaguzi ya TFF, basi akate rufani kwenye Kamati ya Rufani ya Uchaguzi badala ya chombo kimoja kushughulikia mambo mawili,” alisema Tenga.
 
Kuhusu kuondoa nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais wa TFF, kiongozi huyo alisema suala hilo lilitokana na uamuzi wa Mkutano Mkuu uliopita kuwa Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza ziendeshwe na chombo huru.
 
“Baada ya hapo Kamati ya Utendaji iliziambia klabu kuwa tunaunda Kanuni za Kuendesha chombo huru cha ligi, tunaomba mapendekezo yenu. Na ndipo walipotuletea mapendekezo yao kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi atoke kwenye klabu sita za juu na kwamba kiwango cha chini cha elimu kiwe Cheti cha Elimu ya Kidato cha Nne kama ilivyo kwenye katiba,” alisema.
 
“Maana yake ni kwamba sifa hizo hazikidhi utashi wa kikatiba wa sifa za mgombea wa nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais wa TFF ambazo ni Elimu ya Chuo Kikuu, lakini klabu zikasema hazina haja na nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais na ndio maana tunaomba ridhaa sasa ya kuondoa nafasi hiyo.”
 
“Napenda kusema jambo hili ni la maendeleo na hakuna hata moja ambalo si la maendeleo. Tumepata barua kutoka Kagera ikieleza kuwa utaratibu huu haufai, Katibu Mkuu amepata na atawajibu. Pwani nao wameomba ufafanuzi na tutatoa waraka wa ufafanuzi kwa wote.
 
“Watu wana haki ya kuhoji na sisi ni wajibu wetu kuwaelimisha. Ombi langu ni tushirikiane ili twende kwenye mkutano mkuu wetu unaokuja ili tuchaguane. Tukichaguana tutakuwa tumetimiza jambo muhimu kweli kweli.”
 
Tenga pia aliwasihi wajuimbe wa Kamati ya Utendaji kuendelea na jitihada za kuelimisha wajumbe ili waridhie mabadiliko hayo na shughuli za maendeleo ya mpira wa miguu ziendelee kama kawaida.

No comments:

Post a Comment