Na Mwandishi Maalumu
TIMU ya Taifa (Taifa Stars) imeingia kambini jana
jioni (Desemba 12 mwaka huu) jijini Dar es Salaam kujiandaa kwa mechi ya kirafiki
ya kimataifa dhidi ya mabingwa wa Afrika, Zambia (Chipolopolo) huku Kocha Kim
Poulsen akimjumuisha tena katika kikosi hicho kipa Deogratias Munishi ‘Dida’.
Akizungumza na Handeni Kwetu, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Boniface Wambura, alisema Poulsen amemjumuisha tena Munishi kwenye kikosi
hicho kuziba nafasi ya Mwadini Ally, kutokana na kubanwa na timu yake ya Azam inayokwenda kushiriki mashindano maalumu nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya
Congo (DRC).
Wachezaji wote wengine walioitwa Taifa Stars
inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager wamesharipoti kambini hoteli ya Tansoma,
na timu imeanza mazoezi leo asubuhi (Desemba 13 mwaka huu) Uwanja wa Karume, na
jioni itafanya mazoezi kwenye uwanja huo huo.
Kuanzia kesho jioni (Desemba 14 mwaka huu) itafanya
mazoezi Uwanja wa Uwanja wa Taifa wakati mazoezi ya asubuhi yataendelea kuwa
Uwanja wa Karume. Wachezaji ambao bado hawajaripoti kambini ni Mbwana Samata na
Thomas Ulimwengu wanaocheza mpira wa kulipwa nchini DRC.
Mechi kati ya Taifa Stars na mabingwa hao wa Afrika
itachezwa Desemba 22 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa. Kocha wa Chipolopolo,
Herve Renard ameshataja kikosi chake cha wachezaji 24 kwa ajili ya mechi hiyo.
No comments:
Post a Comment