Pages

Pages

Tuesday, December 04, 2012

SIWEZI KUVUMILIA




Wameshaanza usajili wao wa magazeti

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NISHAZOEA kuona wadau wa mpira wa miguu hapa nchini, hasa wa Simba na Yanga wanafanya usajili wao kwa kupitia magazeti. Utaona vichwa vya habari vya kila aina, vinavyohusu wachezaji husika.

Msemaji wa Simba, Ezekiel Kamwaga pichani.

Eti wanafanya usajili wa kufa mtu. Mara fulani kutua kwa mbwembwe. Mwingine anasema, fulani aingia Simba miguu yote. Haya ni baadhi ya maandishi yanayoandikwa katika magazeti mbalimbali, ingawa mwisho wa siku ni vichekesho.

Ndio, maana utashangaa hao wachezaji wanaopigiwa chapuo au kusajiliwa katika klabu hizo wanavyokuwa si lolote kwa waliosajiliwa kimya kimya. Ndio kusema kuwa, yote yanayotokea ni mzigo mzito kwa kwa timu husika.

Sikatai usajili, maana umeruhusiwa na kanuni zote kuanzia zinazoongoza soka la Tanzania na Afrika kama sio Dunia kwa ujumla. Lakini, usajili huo uwe na mashiko kwa timu zetu kwa ajili ya kucheza soka la uhakika na sio blab la.

Tunahitaji uwezo wa kweli kwa wachezaji wanaosajiliwa kwa mbwembwe na sio kukaa benchi au kucheza bila kuonyesha soka la uhakika. Tunahitaji mchango wa uchezaji wa wachezaji hao kwa ajili ya kuinua soka la Tanzania.

Hii ndio maana siwezi kuvumilia. Siwezi Kuvumilia kwasababu wachezaji wengi wanaokuja kucheza soka la Tanzania kutoka nje au hawa wa wazawa lakini wanaoteka vyombo vya habari, wanapotea ndani ya mwezi mmoja tangu wasajiliwe.

Wapo wengi sana ambao licha ya kuandikwa sana, lakini mwisho wa siku uwezo wao umeelekea kusipojulikana. Angalia, mchezaji kama Abdulrahim Humud ambaye sasa yupo Azam FC. Huyu alipamba vyombo vya habari lakini sasa si kama zamani.

Mchezaji kama Ali Ahmed Shiboli alipamba sana vyombo vya habari lakini alipopotelea kiuwezo haijulikani, ingawa tunafahamu kuwa anachezea timu ya Polisi ya Morogoro kwa sasa.

Wapo watu kama Jamal Mba. Huyu aliandikwa sana hadi kupelekea kusajiliwa na timu ya Yanga, lakini matokeo yake ikawa bure kabisa. Kwanini? Haya ni mambo yanayohitaji kuyazungumzia ili viongozi wa timu hizi wafanye usajili wenye akili.

Wasifanye ili mradi tu, maana mwisho wa siku hasara inabaki kwa timu zao, ukizingatia kuwa wana wachezaji wasiojiweza na wanaopata mshahara wa bure kabisa. Huu ndio ukweli na lazima watu waukubali kwa ajili ya maendeleo ya michezo.

Niliowataja ni mfano tu kwa wachezaji ambao majina na uwezo wao uwanjani ni tofauti kabisa, hivyo kunahitaji mpango mzuri kwa ajili ya kuhakikisha kuwa wanaosajiliwa katika timu hizo wafanye kazi kama inavyotakiwa.

Bora hata wachezaji wa nyumbani. Lakini mchezaji wa nje kuja Tanzania kuuza sura tu ni ufujaji wa pesa, ukizingatia kwamba wanalipwa fedha nyingi kama walivyotishia katika upatikanaji wao, kiasi cha kuandikwa sana magazetini.

Nasema hivi maana hali hii itazidi kuharibu maendeleo ya michezo, ukiwamo mpira wa miguu, maana wanaosajiliwa hawaonyeshi soka la uhakika licha ya kupewa mishahara na matunzo mengi kutoka kwa timu zao.

Tuamke sasa kwa ajili ya kuokoa soka letu linalozidi kuanguka siku hadi siku kutokana na utendaji mbovu na usajili wa majina tu, huku wanapoingia uwanjani pumzi hawana, ufundi wa kucheza soka hawana, utashangaa mshahara mnono anaupata kwa sababu gani?

Kwa bahati mbaya, matatizo haya yapo sana katika timu zetu za Simba na Yanga, ambazo kwa kawaida ndio wanaouza magazeti kila siku ya Mungu. Hawa wataandikwa sana kwa mitindo ya kila aina, ingawa mwisho wa siku ni bure kabisa.

Kinachoonekana si kile kilichotarajiwa na watu wengi, ukizingatia kwamba waliaminishwa kuwa yeye ndio kila kitu na timu yake itavuna mazuri kutoka kwake. Huu ndio ukweli wa mambo.

Tunatakiwa tuwe makini katika utendaji wetu wa kazi. Vinginevyo ni hasara kwa Taifa, ukizingatia kuwa soka uwanjani halionekani.

0712 053949
0753 806087

No comments:

Post a Comment