Pages

Pages

Saturday, December 29, 2012

Simba wapigwa 3-0 na Tusker leo Taifa


Kiungo wa Simba, Mussa Mudde, akijaribu kupiga shuti mbele ya mchezaji wa Tusker ya Kenya, katika mchezo wao wa kimataifa wa kirafiki uliopiga leo katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam. Katika mchezo huo, Simba walipigwa bao 3-0.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KOCHA Mpya wa Simba, Mfaransa Patrick Liewig, aliyetarajiwa kuwapo uwanjani wakati kikosi hicho kilipomenyana na Tusker FC katika mchezo wa kirafiki kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ameshindwa kutokea uwanjani hapo na kuwaacha midomo wazi mashabiki wa timu hiyo.

Awali katika taarifa yake, Simba ilidai kwamba Liewig angetambulishwa rasmi kuinoa timu hiyo wakati wa mchezo huo, lakini kukosekana kwake ni jambo lililowaacha njia panda mashabiki wa timu hiyo waliofurika kwenye kumshuhudia kocha wao mpya.

Mechi hiyo ambayo ilitarajiwa na mashabiki wa timu hiyo kwamba watashuhudia kikosi kamili kikishuka dimbani ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara itakayoanza mwezi ujao, badala yake ni kikosi B cha timu hiyo ndicho kilichoanzishwa.

Tusker FC ambao siku kadha zilizopita waliinyuka Yanga bao 1-0, waliendeleza makali yao na kuzichapa timu za hapa nchini baada ya kuinyuka Simba mabao 3-0 katika  mchezo wa kirafiki uliofanyika kwenye dimba la Taifa, Dar es Salaam jana.

Mabao mawili ya Jesse Were na moja la Fredrick Onyango yalitosha kuitoa kimasomaso Tusker katika mchezo ambao mashabiki wa Simba walishindwa kupata burudani kutoka kwa nyota wao wa kimataifa kutokana na kutokuwapo katika mchezo huo.

Katika mchezo huo, Simba ilianza kumtumia tena kiungo wake mshambuliaji, Haruna Moshi 'Boban', aliyeingia kipindi cha pili kujaribu kuweka mambo sawa, lakini mambo yaliendelea kuwa magumu kwa kikosi hicho cha Wekundu wa Msimbazi.

Boban alicheza mechi hiyo akitokea kwenye adhabu ya kufungiwa mechi kadha za duru la kwanza la Ligi Kuu Bara kwa madai ya kwamba ni utovu wa nidhamu.

Kama timu tumeona hilo sio tatizo na kwamba kocha wetu mtu atatua hapa nchini Jumatatu. Kuhusu wachezaji wengi, Okwi (Emmanuel) na kipa wetu Abel Dhaira na Sunzu (Felix) watatua hapa nchini kesho (leo).

Kuhusu wale wachezaji waliokuwa kwenye timu ya taifa, Kapombe (Shomari), Ngassa (Mrisho) na wengineo watajiunga rasmi na timu Jumatatu.

Katika mchezo wa jana, Simba ilijaribu kufanya mabadiliko kadha ya kuwaingiza wachezaji wake, Boban, Edward Christopher, Nassor Chollo, Emily Isyaka, Salum Kinje, Jonas Mkude na Ramadhan Singano, lakini hakukuwa na mabadiliko yoyote na hivyo hadi mwisho wa mchezo, Simba ilikubali kipigo.

Simba: William Mwete, Haruna Shamte, Paul Ngalema, Hassan Hatibu, Komain Keita, Mussa Mudde, Haroun Athuman, Abdallah Seseme, Abdallah Juma, Ramadhan Chomo, Kiggy Makassy.

Tusker FC: Samwel Odhiambo, Luje Ochieng, Jeremiah Bright, Mana Odhiambo, Joseph Shikokoti, Khalid Aucho, Edwin Ombasa, Fredrick Onyango, Jesse Were, Robert Omonuk. Refa: Hashim Abdallah kutoka Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment