Pages

Pages

Monday, December 10, 2012

Serikali imepoteza uaminifu kwa wananchi


Rais wa Jamhuli ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete
 
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
YAPO mambo mengi yanayoifanya Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ishindwe kueleweka na kuheshimika kwa wananchi wake, likiwamo hili la watendaji wake kufanya kazi chini ya kiwango.
 
Watendaji hao ambao wameaminiwa na kupewa nafasi hizo, wanawaangusha mabosi wao. Katika hili kila mmoja ni muathirika kwa wakati wake.
 
Hata wale wanaoshika nafasi hizo kisiasa, hasa wabunge, mawaziri na manaibu waziri, baadhi yao wamekosa uaminifu kwa watu wao, licha ya kuamini kuwa watawaletea mafanikio.
 
Uamuzi wao mara nyingi huwa wa mashaka. Wanawaacha ndugu zao wakishindwa kuelewa kwanini wamezaliwa katika nchi hii, inayojipambanua kuwa ina utawala bora na demokrasia ya kueleweka.
 
Watendaji wengi wamekuwa wakifanya uamuzi ambao wakati mwingine huwa na walakini ndani yake. 
 
Wanabaki wakilalamikiwa au kuogopwa kama miungu watu, hivyo kuwa mwiba mchungu kwa Serikali ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye hatasahau uongozi wake kuwa na misuko suko ya kila aina.
 
Nimelazimika kuanza hivi baada ya kugundua kwamba idadi kubwa ya wananchi wamekosa imani na nchi yao na hamu ya kuendelea kuithamini kutokana na viongozi hao kuweka mbele maslahi yao binafsi, huku wakishindwa kuzitatua kero kubwa na ndogo.
 
Kwanini nasema hivyo? Tanzania kila siku ya Mungu inatawaliwa na migomo isiyokuwa na kikomo. Katika hilo, wengi wanapoteza maisha na wengineo kuacha wajane na watoto wa mitaani.
 
Hili halitaji elimu ya Chuo Kikuu kuona kwamba kadhia hiyo inaacha pigo kubwa katika jamii zetu. Mara nyingi wanaosumbuliwa na matatizo hayo ni wale wasiokuwa na kipato kikubwa.
 
Wale ambao hata mlo wa siku moja kwao ni tatizo kubwa, hivyo viongozi wanaowangiza katika mikataba tata, isiyokuwa na faida na nchi, hakika wanawaumiza walalahoi, maana fedha nyingi zinatumiwa bila sababu za msingi, wakati faida inayopatikana, inaingia kwenye mifuko ya baadhi ya wakubwa serikalini.
 
Masikini wanabaki wanalia. Wanaishia kulalamika. Hawajui la kufanya, hasa wanapokumbuka kuwa kilio cha samaki, machozi yanakwenda na maji.
 
Kwa mfano, hakuna asiyetaka jambo la maendeleo katika sehemu yoyote ile Tanzania. Lakini, tunapozungumzia hayo maendeleo, tuhakikishe kuwa yanapatikana kwa haki, ushirikiano na maelewano kwa wote, ukizingatia kwamba nchi hii ni yetu wote.
 
Wale wanaoletewa maendeleo hayo, lazima walindwe, wasibuguzwe katika nchi yao. 
 
Na inapofikia wanatakiwa wahamishwe kwa makubaliano ya kuwalipa, basi wapewe haki zao kulingana na thamani ya majengo yao pamoja na mimea yao.
 
Kwa bahati mbaya, baadhi yao wapo tayari kutoa roho za wenzao, maana wameamua kufanya harakati za kuleta maendeleo kwa vurugu, manyanyaso, wakiwa na virungu pamoja na silaha nyingine lukuki, kama njia ya kujihami itakapotokea purukushani.
 
Kupo kunapotokea vurugu na pia kule kunapokuwa na utulivu katika operesheni ya aina mbalimbali, ikiwamo ile ya kuhamishwa katika eneo moja kwenda lingine kwa faida inayokusudiwa na serikali.
 
Kwa miaka kadhaa sasa kumekuwa na kutoelewana kati ya serikali na wananchi wa Kwembe, Manespaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
 
Katika eneo hilo, zimeandaliwa zaidi ya heka 3800 ambazo kwa mujibu wa wenyeji, kunatakiwa kujengwe Chuo cha Muhimbili na shughuli nyingine za kijamii.
 
Sawa, ni jambo zuri. Hakuna asiyetaka maendeleo, maana kama chuo kitakamilika, watasoma Watanzania wenzetu hivyo tunalipokea kwa furaha kubwa.
 
Ila, baada ya mvutano wa muda mrefu, hatimae nyumba zaidi ya 86 zimevunjwa wiki hii, wakati malipo yao yakiwa madogo na hayalingani na maisha ya leo.
 
Mtu mwenye nyumba moja ya kawaida yenye mimea kama vile miembe, michungwa na mingineyo kupewa Sh 400,000 huko ni kumuonea.
 
Wapo waliopewa Sh Milioni 4 licha ya kuwa na nyumba nzuri za thamani sambamba na mimea.
 
Uonevu mkubwa unafanywa na serikali na dhambi hii hakika inaweza kuwaathiri siku za usoni.
 
Watu wanalalamika kwa kukandamizwa na serikali yao, tena ile wanayoiweka madarakani. Wanapoteza imani nayo, maana maendeleo yanayotakiwa yanasakwa kwa kupitia migongo yao.
 
Hawaonewi huruma kamwe. Wananchi wa aina hiyo waende wapi? Shida zao nani wa kuzitatua? Hili lazima watu walibaini, maana tunapoelekea ni kubaya na ipo siku watafanya uamuzi mgumu.
 
Serikali ya CCM isikimbilie tu kujivua gamba kwa baadhi ya wanasiasa wao, bali pia wale wanaoshika vitengo nyeti, wawe na mioyo ya kibinadamu.
 
Wakuu wa wilaya ambao ndio wawakilishi wa Rais wafanye kazi yao kama inavyotakiwa.
 
Wasipokuwa makini, chuki kwa serikali yao itakuwa ya aina yake na itafikia wakati hawatakubali ushauri wa aina yoyote kutoka kwa mtu yoyote.
 
Nilikuwapo katika oparesheni ya kubomoa nyumba katika Kata ya Kwembe. Nilichokiona, haki haijatendeka kwa wananchi waliobomolewa nyumba zao.
 
Ndio wamelipwa kiasi kidogo cha pesa, lakini fedha hizo haziwezi kuwasaidia wajenge sehemu nyingine tofauti na pale walipovunjiwa, ukizingatia kwamba hawajapewe eneo lingine kwa ajili ya kuanza maisha mapya.
 
Maisha ni magumu. Watanzania wanaishi kwa kubahatisha, huku wachache wanaofanikiwa kujenga, hulazimika kulala njaa ili wasimamishe vibanda vyao.
 
Maendeleo yanapobuniwa, huona wao ndio wahusika, hivyo kuhesabiwa vijisenti vya kula kahawa na kupewa bila kuonewa huruma.
 
Hii ni dhuluma ya wazi wazi kwa serikali. Dhambi hii lazima ikemewe, maana kuna wakati wananchi watachoka kama wanavyochoka kila siku na kuanza kupaza sauti zao juu kwa kisingizio cha ‘Nguvu ya Umma’.
 
Wanaona huko ndipo ambapo watu wameamua kujitoa kwa walalahoi, wale wanaodhulumiwa haki zao kila wakati, hivyo kuwapa uchungu.
 
Tembelea kila kona ya nchi hii utagundua malalamiko kwa serikali ni mengi mno. Ndio, wapo watakaosema serikali haiwezi kukwepa lawama.
 
Sawa, ila hali ikiendelea hivi, hakika itakuwa balaa. Hawa wakimka watachukua uamuzi ambao nchi nzima tutashindwa kuwaelewa.
 
Je, ni kweli kuwa wanaolalamika wengi wao ni wanasiasa na hawana hoja? Hata wale wanaonyonywa katika migodi pia hawana hoja?
 
Nao ni wanasiasa? Wale wanaomenyeka katika machimbo ya dhahabu na bado wanatakiwa wasichukuwe fedha zao kwenye mifuko ya pensheni hado baada ya miaka 55?
 
Hii ni hatari. Hakuna juhudi za kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania zaidi ya kubuni mbinu za kuwakandamiza wale wenye kipato cha chini. Wanakandamizwa na kuwatoa manyozi ya damu.
 
Wanajitahidi, ila mwisho wake huchoka na kukubali wapoteze maisha, maana wameshindwa kuipata hata ile haki yao ya msingi.
 
Hii sio haki. Maendeleo hayawezi kupatikana kwa kuwakandamiza zaidi walalahoi, wakati nchi ina rasilimali nyingi zinazoweza kuingiza fedha, endapo viongozi watajipanga na kufanya kazi kwa ajili ya Watanzania wote na sio wachache wao.
 
Serikali imepoteza mvuto kwa wananchi wake. Haiaminiki tena kwa watu wake, ndio maana wengi wao wameanza kuamka na kukimbilia katika vyama vya upinzani.
 
Kwa bahati mbaya, uamuzi wao huo unaonekana kama vile wanajisumbua, maana baadhi yao hudhani hakuna chama kizuri zaidi ya CCM.
 
Chama chenye historia kubwa na Taifa hili, ingawa kwa siku za karibuni, watu wake wameanza kuingia mahali sipo.
 
Wanakiacha chama kikishambuliwa na wabaya wake, maana wao wenyewe wameacha kufanya kazi kwa ajili ya chama na nchi kwa ujumla wanahubiri siasa za chuki na wale wengine wanaona uongozi bora ni kuwanyonya walalahoi, jambo ambalo si kweli.
 
Lengo lao ni kuangusha chama na serikali yake, ndio maana wanaposhauriwa, hukataa na kusema eti wanaolalamika ni wanasiasa kutoka vyama vya upinzani wasiokuwa na hoja, huku wakifananisha na robo ya sukari ndani ya bahari.
 
Kauli kama hizi kwenye siasa ni mbaya. Haziwezi kukiokoa chama zaidi ya kukiangusha, hasa katika kipindi hiki kigumu kwa siasa za Tanzania, maana katika siasa somo la kutoa wanachama ni baya kuliko lile la kuongeza wanachama na wafuasi wapya.
 
Na katika hilo, ni rahisi kupunguza wanachana na wafuasi wa zamani kuliko kuongeza wapya, hasa kwa CCM, kinachokaliwa kooni na vyama vya upinzani.
 
Kipindi ambacho wapinzani hasa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) muda wote wanashambulia kwa kufanya mikutano katika mikoa mbalimbali ya Tanzania.
 
Huko kote wanahubiri mabaya ya serikali ya CCM, wakisaidwa na wenzao CUF, chama ambacho kinaunda serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, maarufu kama (SUK) chini ya Rais wake, Dk. Mohamed Ali Shein.
 
Kila mmoja awe na nia ya dhati ya kutatua kero za Watanzania, huku wakiweka mbele ubinadamu na kuacha kuwakandamiza wananchi.
 
Serikali ipo kwa ajili ya kuwaongoza Watanzania wote, hivyo katika hili lazima ikae na kujisahihisha, maana hali inavyokwenda, kuna siku lawama hizi zitawaumbua viongozi wake, hasa wanaotoka katika chama tawala, chenye hamu ya kutawala milele, katika upepo huu wa mabadiliko ya kisiasa.
 
Mungu ibariki Tanzania.
 
0712 053949
0753 806087
 
Makala hii iliwahi kutumika katika gazeti la Mtanzania.
 

No comments:

Post a Comment