Pages

Pages

Monday, December 31, 2012

SALAMU ZA MWAKA MPYA



BY KAMBI MBWANA
NATUMIA fursa hii kukushukuru wewe ambaye umekuwa bega kwa bega tangu kuanzishwa kwa blog hii ya Handeni Kwetu. Ingawa blog hii ilianzishwa rasmi mwaka jana mwishoni, lakini ilinichukua miezi takribani 10 kuitendea haki.

Kwanini nasema hivyo? Kutokana na kubanwa na majukumu mengine, iliniwia vigumu kuingiza kazi mbalimbali kwa ajili ya kuwapa uhondo wasomaji wangu, ambao licha ya changamoto hizo lakini walikuwa na mimi.

Wakati nausubiria mwaka mpya

Mpenzi msomaji, najiona kuwa ni mwenye bahati sana. Kwani katika kipindi cha wiki ya mwisho ya mwezi Desemba, tumeweza kuingiza wasomaji wapya zaidi ya 4000, kiasi ambacho ni kikubwa mno katika blog inayochipukia.

Naamimi wingi huo unatokana na kufanya kazi kwa moyo nikiwa na melengo zaidi ya kupeana habari mbalimbali. Ndugu msomaji wangu, napenda kutangaza kuwa blog hii haichagui.

Nimekuwa mwepesi kuandika kila ninachoweza. Na kuanzishwa kwa blog hii kumetokana na kuwa na malengo mawili makuu. Lengo la kwanza ni kutafuta mahali kwa kusemea, nikiona kuwa kazi ya uandishi wa habari, nipo kwenye vyombo vya watu vya habari.

Hivyo kama wakati mwingine naweza kubanwa na sera ya kampuni, ingawa changamoto hizo sijakutana nazo hadi muda huu, basi blog ya ‘Handeni Kwetu’ itanipa nafasi ya kusema kila ninachojisikia ili mradi tu nisivunje sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuzungumza na wasomaji wetu na ujumbe wangu kufika kwa wakati.

Lengo la pili ni kutafuta namna gani naweza kuwaunganisha Watanzania wanaoishi ndani na nje ya nchi, bila kusahau wakazi na wananchi wa wilaya ya Handeni yenye changamoto nyingi.

Nashukuru kwa dhati. Nashukuru maana nimepata mwangaza kugundua kuwa kazi zangu zinapendwa. Na ndio maana nimekuwa mwepesi kuandika makala za aina mbalimbali, ikiwamo kolamu ya ‘Mgodi Unaotembea’, ‘Mambo Fulani Muhimu’, ‘Siwezi Kuvumilia’ na zote ninazoandika katika uwepo wa kazi yangu ya uandishi wa habari na uchambuzi wa makala zangu ambazo pia hupatikana katika gazeti la Mtanzania, linalochapishwa na Kampuni ya New Habari 2006 Ltd, yenye maskani yake jijini Dar es Salaam Tanzania.

Habari za aina mbalimbali za michezo, siasa, afya, burudani na sanaa kwa ujumla, bila kusahau biashara, afya na nyinginezo. Katika kulisema hilo, napenda kusema mwaka mpya wa 2013 nitakuwa makini zaidi.

Nitafanya kazi kwa moyo wote. Wewe kama mdau wa ‘Handeni Kwetu’, usisite kunishauri na kunikosoa kwa njia mbalimbali, ikiwapo safu iliyoandikwa TOA MAONI YAKO KUHUSU HANDENI KWETU.

Kwakuwa sisi ni marafiki na ndugu moja, usisite pia kunitumia habari yoyote, picha unayoona inafaa kuonwa kwenye blog ya ‘Handeni Kwetu’ ili iwe elimu kwa wasomaji wote.

Napenda kumaliza kwa kumshukuru tena Mungu pamoja na wewe kwa kuniunga mkono katika kipindi chote cha mwaka 2012 na mwaka mpya wa 2013, huku nikiamini kuwa tutaendelea kuwa pamoja wakati wote.

Asanteni sana na tuendelee kushirikiana.





No comments:

Post a Comment