Pages

Pages

Thursday, December 20, 2012

Ngwasuma kukamua Arcade House Krismasi



 Nyosh el Sadaat

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WAKALI wa miondoko ya dansi ya FM Academia, maarufu kama ‘Wazee wa Ngwasuma’, Desemba 25 wanatarajia kutoa burudani katika Ukumbi wa Arcade House, Mikocheni katika Sikukuu ya Krismasi.

Shoo hiyo itakuwa ya aina yake, huku ikiporomoshwa na magwiji wa muziki wa dansi nchini, akiwamo Patchou Mwamba, Nyosh El Sadaat na wengineo wenye lengo la kuonyesha uwezo wao.

Akizungumza jijini leo mchana, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa bendi hiyo, Kelvin Mkinga, alisema kwamba maandalizi ya maangamizi ya burudani hiyo yamekamilika.

Alisema wanamuziki wake wote wote wapo kwenye uwezo wa juu kwa ajili ya kuwapatia raha mashabiki wao katika Ukumbi huo wa kisasa.

“Huu ni wakati wa kufanya mapinduzi katika tasnia ya muziki wa dansi hapa nchini, hivyo naomba wadau na mashabiki wetu waje kwa wingi Arcade siku ya Krismasi.

“Nyimbo zetu zinazopendwa na mashabiki wetu zitaimbwa, huku tukiamini kuwa tunashiriki kwa dhati kufurahia na kumuomba Mungu tuumalize mwaka salama,” alisema Mkinga.

Baadhi ya nyimbo zinazopendwa na watu wengi ni pamoja na Heshima kwa Mwanamke, Anna, Vuta Nikuvute, Otilia na nyinginezo zinazofanya vyema kutokana na kuimbwa kwa ufundi wa aina yake.

No comments:

Post a Comment