Pages

Pages

Thursday, December 20, 2012

Ngoma hii ya Chadema haitakesha kamwe



MGODI UNAOTEMBEA
 Katibu Mkuu Chadema, Dk Wilbrod Slaa

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KUKIKOSOA Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kunahitaji moyo wa uzalendo na kujitoa kwa nguvu zote, hasa ukijua kuwa kadhia utakayoipata kutoka kwao ni kubwa mno.

Ni dhahiri, Chadema kama vilivyokuwa vyama vingine vya siasa, nao hujiona kwamba katika kila wanalofanya hapa chini ya jua, ni jema.

Akijitokeza mtu wa kuwaonyeshea kidole, wataanza kulalama na kusema bila ukomo. Watasema yasemwayo yanametokana na matakwa ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
 Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye

Kuna siku moja niliwahi kufanya mazungumzo kwa kupitia simu na Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene na kugundua kuwa kila ambalo nimekuwa nikifanya kwa maslahi ya Taifa, aliona si mazuri, hasa kama nimekosoa chama chao.

Kwa bahati nzuri nakumbuka makala nyingi nilizowahi kuandika, iwe za kuikosoa CCM, Chadema au Chama Cha Wananchi (CUF), zimekuwa zikielezea tatizo na suluhu yake, ukizingatia kwamba vyama hivi ndio vinavyokubalika kwa Watanzania wengi.

Makene alifanya hivyo kwakuwa ana haki na wajibu wa kuhoji juu ya mwenendo wa waandishi na wachambuzi wa siasa, maana wapo kwenye meza yake.

Hata hivyo, kati ya majibu niliyompa kwa wakati huo, nashukuru yalitoka katika kichwa changu na ukweli ni kuwa ‘Mgodi Unaotembea’ haujaelemea kwenye chama chochote cha siasa na ndio maana unasimama kwenye ukweli.
Wafuasi wa CCM
 
Kwanini nimeanza hivi? Chadema ni dhahiri ngoma yao haitakesha kamwe. Nasema haya kwakujua kuwa, baadhi yao wamekuwa wepesi sana kucheza wimbo unaopigwa na vyama vingine vya siasa, hasa CCM na CUF.

Chadema ni rahisi sana kuyumbishwa hata kwa sababu nyepesi, hivyo kuonyesha kuwa uwezo wao, upeo wao wote unaweza kuamuriwa na kada au kiongozi mmoja tu kutoka kwenye chama kimoja cha siasa nchini.

Ndio, maana hivi sasa Chadema wanashikana mashati baada ya kauli moja tu ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Moses Nnauye. Nape alisema jijini Mwanza kuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa ana kadi ya CCM.
 Wafuasi wa CUF

Sawa huenda kweli anayo. Lakini wote hawajui kuwa Slaa ana kadi ya CCM. Nape alisema kwakuwa ndio wakati wake. Yeye ndio Katibu wa Uenezi na alifanikiwa kueneza, maana aliyosema yanaleta balaa kwenye chama hicho.
 Wafuasi wa Chadema

Viongozi makini na wanachama wanaojitambua, hawapaswi kuanza kuparuana wakimtaka Katibu wao, Slaa eti ajiuzulu. Kwanini? Kwamba ana kadi ya CCM? Hivi Chadema hawajui kuwa Slaa alikuwa kada wa CCM?

Sawa alipaswa kuirudisha au kuichoma moto kama wanavyotaka wao wanaopenda siasa za kujionyesha majukwaani, lakini hii njia wanayopita ni sahihi kwa ajili ya chama chenye nguvu na malengo ya kushika dola?

Pia tujiulieze maswali. Ingekuwaje Slaa angekuwa rais wa Tanzania baada ya Uchaguzi uliofanyika mwaka 2010 na  kumsumbua Rais wa Tanzania, Dk Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM?

Je, Nape kama kawaida yake angesema kuwa Slaa ana kadi ya CCM? Wanachama na wafuasi wa Chadema leo hii pia wangetaka ajiuzulu?

Maswali haya najiuliza baada ya kugundua kuwa licha ya wapinzani kukubalika kwao, vichwa vyao, nafasi zao, upeo wao kisiasa bado ni mdogo kiasi cha kushindwa kufahamu masika au kiangazi katika maisha ya vyama vyao.

Kumbe Nape ni hodari mno kuliko vichwa vya umoja wa vijana wa Chadema na viongozi wengine, hasa kwa hoja yake hiyo inayoweza kusababisha chama hicho kusambaratika kwa kasi.

Bila hata kusimama upande mmoja, CCM wenyewe wanajua kuwa kichwa cha Slaa ni mahiri na kinaweza kuwasumbua wakati wowote. Katika hilo, wapo wanaopewa jukumu la kuhakikisha kuwa Chadema haitulii.

Na kwa vipi isitulie? Ni kuhakikisha kuwa kinavurugika kuanzia katika nafasi ya Katibu Mkuu, ambaye ni dhahiri Watanzania waliokuwa wengi wanazidi kuona Slaa anafanikiwa kuongoza Watanzania katika Uchaguzi ujao.

Kwa kufanikisha madai yao ya Slaa ajiuzulu kwa sababu eti ana kadi ya CCM, Chadema itamchagua nani kurithi mikoba yao? Ndio wapo, lakini watakuwa salama? Je, atakayerithi hajatokea katika mikona ya CCM?

Ukiangalia suala hilo, utagundua kuwa ni wazi kuwa chama kitakwenda mwisho wake kitaanguka. Kwa kuanguka kwake leo au kesho kwasababu ya kuanzishiwa zogo na kulifanyia kazi kama majuha, ngoma yao haitakesha.

Wahenga wa zamani walisema siku zote kuwa ngoma ya kitoto haiwezi kukesha. Ni kweli kabisa. Chadema wanaweza kufuata nyayo hizo. Kwa kuwategemea wafuasi na makada au viongozi wa CCM, wakiongozwa na Nape.

Mwishoni mwa wiki, Baraza la Vijana la chama hicho (BAVICHA), kwa kupitia Katibu wa mkoa wa Mwanza, Salvatory Magafu, lilivalia njuga suala la kadi ya Slaa na kutangaza maandamano ya kumng’oa madarakani.

Kauli ya Magafu ilipingwa vikali na Mwenyekiti wake, Liberatus Mlebele, kwa madai kuwa sio msemaji wa umoja huo, ambao kwa hakika ni msimamo wa kunyoosheana vidole kutoka kwa viongozi wa chama hicho.

Kwa bahati mbaya, maneno ya Magafu yalizua utata kwa baadhi ya makada na wapenzi wa Chadema, hasa kwa kuyapayukia baadhi ya magazeti na waandishi wao kwa madai kuwa wanafanya kwa nia ya kukiharibu chama chao.

Hii ni tabu sana. Watu wengi wamekuwa wakiangalia walipoangukia badala ya walipojikwaa. Kwa mwendo huu upinzani kushika dola itakuwa ngumu. Kinyume chake CCM itaendelea kuwa watalwa wa Taifa hili.

Wanajua wanachofanya. Wanajua ili kukineemesha chama chao basi ni kuwaimbia wimbo wowote ambao nao bila kujua, wapinzani watauchukua na kuuimba pamoja na kucheza. Hakuna maelewano ya aina yoyote.

Na wanajua pia baada ya Slaa kupotea litaibuka tena la mbio za urais za Mbunge wa Kigoma, Zitto Kabwe, Freeman Mbowe na Slaa. Njia hii inajenga uhasama kwa viongozi wa juu wa Chadema, ambao nao wana matawi yao.

Na kama maelewano yanakosekana, nani anaweza kujenga hoja ya kukijenga chama wakati hakuna anayempenda wala kumheshimu mwenzake? Sawa, lakini njia hii ni tunu kwa CCM. Kila mwana CCM anafurahia matokeo ya sasa.

Mvurugano uliopo ni ishara kuwa ngoma ya kitoto haikeshi na ndoto ya upinzani kushika dola kwa vyama hivi bado. Watanzania wataaminishwa uongo, maana ukiangalia mfumo mzima wa Chadema katika kila mkoa utagundua msigano usiokuwa wa lazima.

Na kwakuwa wataalamu kutoka CCM wanaweza kuwachezea wanavyotaka, ni dhahiri kila litakalosemwa litakuwa kubwa na kuwachanganya zaidi wapinzani hao, huku ajenda yao ya kujiuzulu ikikolezwa zaidi.

Tunasema hili kwakuwa baadhi yao tunajua kuwa kwa kuwapo vyama vya siasa vya upinzani, walau yapo maendeleo makubwa kwa Taifa hili, maana inajulikana wapinzani ndio wakosoaji wa serikali iliyokuwapo madarakani.

Makala ya Mgodi Unaotembea, huchapishwa na gazeti la Mtanzania kila Jumatano na Jumapili.

kambimbwana@yahoo.com
0712 053949
0753 806087


No comments:

Post a Comment