Pages

Pages

Thursday, December 20, 2012

Injili yawapika waimbaji wake



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
CHAMA Cha Muziki wa Injili Tanzania, jana kimeandaa kikao cha pamoja na waimbaji wake kwa ajili ya kuangalia changamoto zinazowakabili, wakishirikiana na Mfuko wa Pensheni wa LAPF na Grace Production inayotengeneza bidhaa mbalimbali za vipodozi.

Mkutano huo ulifanyika jana katika Hoteli ya Wanyama iliyopo Sinza Mori, jijini Dar es Salaam, huku ukikutanisha wasanii wengi akiwamo Bahati Bukuku.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam katika kikao hicho cha pamoja cha kujadili maisha ya wasanii miaka ya baadaye, Rais wa Chama hicho, Addo November, alisema kwamba maisha ya wasanii hayaonyeshi kesho nzuri, hivyo wameamua wakutane kulijadili jambo hilo.

Alisema kumekuwa na tatizo kubwa la wizi wa kazi za wasanii huku serikali yenyewe ikiwa haina majibu ya moja kwa moja, hivyo kwa kufanya kikao hicho wakiwa na wadau wao, wakiwamo Grace Production, LAPF na wengineo wanaamini watakuwa na jibu la msingi kwa watu wote.

“Huu ni wakati wa kuangalia namna gani tunaweza kufanya mambo yenye kuleta maendeleo kwa watu wote wakiwamo wasanii ambao baadhi yao wanaishi kwa tabu kutokana na kazi zao kunufaisha watu wengine.

“Naamini hapa watapewa elimu kubwa ya kuhusu maisha yao ya leo na kesho, ukizingatia kwamba lengo letu ni moja la kuwakomboa wasanii nchini,” alisema.

Naye mwimbaji mahiri wa muziki huo nchini, Bahati Bukuku, aliitaka serikali kuingia kwa undani zaidi kwenye matatizo yao badala ya kuwaacha kama walivyo.

Bahati kwa sasa anatamba na wimbo wake wa Dunia Haina Hurumu huku ukifanya vyema katika chati za muziki huo hapa nchini na kumuweka juu zaidi.

No comments:

Post a Comment