Pages

Pages

Wednesday, December 12, 2012

IDDI JUMA: MWENYEKITI MPYA CCM KILIMANJARO ALIYEPANIA KUVUNJA MAKUNDI

  
Na Fadhili Athumani, Moshi

05, Desemba

CHAMA cha Mapinduzi kama tunavyofahamu katika siku za hivi karibuni ilikuwa katika hekeheka za kufanya uchaguzi wa ndani katika ngazi za mikoa na ule wa kitaifa uliofanyika katika mkutano mkuu jijini Dodoma na Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania akachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM kwa mara nyingine tena kwa kishindo.

Katika chaguzi hizo mikoani imetumia fursa na haki yao kikatiba kwa mujibu wa katiba ya chama tawala kuwachagua watu wanaofaa kuwaongoza kwa ufanisi mkubwa na wenye uwezo wa kutekeleza sera na ilani ya chama na mmoja wao ni Mwenyekiti Mpya wa chama cha Mapinduzi mkoa wa Kilimajaro, Iddi Juma.

Kwa miaka mingi sasa mkoa wa Kilimanjaro umekuwa ukichukuliwa kama moja ya ngome ya chama cha mapinduzi CCM sifa ambayo hata hivyo kwa miaka ya hivi karibuni imeanza kutoweka huku majimbo mengine yakitwaliwa na vyama vya upinzani.

Mzimu huu umekuwa ukikiandama chama tawala katika chaguzi za hivi karibuni huku upinzani mkubwa ukitoka katika chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambayo kwa sasa ndiyo inayoongoza sehemu kubwa ya jimbo la Moshi ikiwa ni pamoja na Baraza la Madiwani kwa maana ya Manispaa.

Kwa kutambua hilo chama cha Mapinduzi (CCM), mkoa wa Kilimanjaro, kimeona haja ya kufanya mabadiliko na kufanya maamuzi ya kijasiri na kumchagua Mwenyekiti mpya na kumpa nafasi Iddi Juma kuwaongoza katika juhudi za kuukomboa mkoa na shubiri ya upinzani ambayo imeanza kikitishia CCM mkoani Kilimanjaro.

MTANZANIA ilifanya mahojiano na mwenyekiti huyo katika ofisi zake zilizopo katika jingo la makao makuu ya chama cha Mapinduzi mkoa wa Kilimanjaro, na hapa Iddi Juma pamoja na mambo mengine mengi anaweka wazi mikakati yake katika kukiinua na kukiimarisha Chama tawala mkoani hapo.
Juma anainisha baadhi ya malengo yake na kusema moja ya kazi atakazozifanya ni kusafisha chama hicho kongwe hapa nchini na katika kuhakikisha hilo linafanyika, katika kikao cha pili cha Halmashauri kuu CCM mkoa wa Kilimanjaro, Juma aliteua wajumbe watatu katika kamati ya Siasa, ambao ni Amina Shamba, Dkt.Steven Moria na Zainah Heshima.

Mwenyekiti huyo anasema ili kuweza kufikia malengo ya kuimarisha chama na kukomboa majimbo ambayo ndiyo kazi kubwa aliyoazimia kuifanya kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, ni lazima uwepo wa ushirikiano katika kila upande, kupendana na uwepo wa uwazi lazima uzingatiwe.

 Anasema Tatizo kubwa la CCM mkaoni Kilimanjaro, upo kwa wanachama wenyewe na kuongeza kwamba katika kipindi kirefu amekuwa akifuatilia mwenendo wa CCM mkoani Kiliamanjaro na kubaini kinachijitokeza hivi sasa dhidi ya CCM, unatokana na wanachama wenyewe ambao anasema baadhi yao ni mandumakuwili.

“Unajua kwa muda mrefu sana hata kabla ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti katika uchaguzi uliomalizika wa Oktoba 18, nimekuwa nikikifuatilia CCM na kubaini miongoni mwetukuna watu waliojisahau, kuna watu mandumakuwili, wenye mapenzi ya kinafiki juu ya chama huku mioyo yao ikiendelea kuhusudu pesa na uongozi.

“Kumekuwa na mjadala kuhusu makundi ndani ya chama, japo watu wengi wamekuwa wakikana ukweli huu, nataka niweke wazi kwamba na ieleweke kwamba miongoni mwetu kuna watu wachache wasio waaminifu na ndio hao hao wanaozunguka kueneza dhana hii potofu ya kuwepo kwa makundi ndani ya Chama.

“CCM tuko shwari, tuko imara na ndio maana hata kwenye uchaguzi wa hivi karibuni wa udiwani CCM ilifanikiwa kuibuka na madiwani 22 kati ya nafasi 27 zilizokuwa zikiwaniwa, kinachotakiwa kufanyika ambacho mimi binafsi nimekuwa nikipigania kila kukicha katika mkoa wetu ni kupembua pumba.

“Lengo letu ni kuona majobmo yote yaliyokuwa chini ya CCM hapo awali yanarudi katika himaya yetu, nitapigana kwa nguvu zangu zote kuhakikisha katika uchaguzi ujao wa 2015 tunashinda majimbo yote hasa jimbo la Moshi mjini, Hai, Rombo na Vunjo,” anasema Juma.

Anasema kwa sasa kinachotakiwa kifahamike a kuheshimika na wanachama wote, ni ukweli kwamba uchaguzi umepita, muhimu sasa ni kubaini kwa ufasaha matatizo, vikwazo na changamoto na kuyatafutia ufumbuzi kwa lengo la kwenda sanjari na kauli mbiu ya Mkutano mkuu wa Nane wa CCM “UMOJA NA USHINDI, UMOJA NI USHINDI”.

Juma anasema ili kuona hayo yanafikiwa , wanachama na viongozi wote ndani ya chama Tawala, wanatakiwa kwa nguvu zote kuyakataa makundi hasi, kukemea na kupinga kwa nguvu zote, unafiki na undumila kuwila na tabia ya kujengeana chuki ndani ya CCM hasa baada ya Uchaguzi.

“Kumekuwa na matukio ya watu kuingia katika misuguanio mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi, kujengeana chuki, sidhani kama tunahitaji kuchukiana, kinachotakiwa ni kuwa kitu kimoja, pale inapobidi pafanyike vikao vya upatanishi na masikizano kwa waliochaguliwa na wasiochaguliwa.

Watanzania tujifunze na kuhimizana kuponya majeraha na kuziba nyufa zilizosababishwa na chaguzi za ndani ya chama, ya kitaifa na yale ya kimataifa, mataifa mengine yameweza, Marekani wameza kwa nini sisi tushindwe?” anasema Juma

Akizungumzia swala la kikao Mwenyekiti huyo anakumbushia na kunukuuu kauli ya Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama aliyoitoa hivi karibuni katika kikao cha kamati ya ushauri ya Mkoa (RCC), kwamba watamishi na baadhi ya viongozi katika ofisi za umma wanafanya kazi kwa mazoea.

Juma anasema tatizo hilo haliko katika maeneo ya utendaji na utumishi tu, bali hata kwenye siasa na hasa Chama tawala, anasema kumekuwa na tatizo la viongozi wengi kutofanya vikao na hata wanapofanya vikao hivyo, vinafanyika kinyemela na mara nyingi hata ajenda zinazojadiliwa hazina mashiko na jamii wala Chama.
“Moja ya mdudu unaotafuna chama chetu ni utabia ya baadhi ya viongozi kugeuza Maofisi, mikutano ya hadhara na Vikao vya Vyama kuwa vijiwe vya umbea na Majung, nadhani ifike muda sasa Viongozi tutambue dhima iliyoko mbele na tutimie vikao kujadili yenye mashiko na jamii na chama.

“Nitafarijika kuona viongozi wa Chama cha CCM, mkao wa Kiliamanjaro watatumia muda mwingi kuhimiza ufuatiliaji kwa ukaribu wa ufanyikaji wa vikao vyote vya chama kwa mujibu wa katiba na kuheshimu maadili na miiko ya chama aliyoiweka Baba wa Taifa, Julius Kambarage Nyerere.

Mwenyekiti huyo hata hivyo anasema kuwa, kwa miaka takribani 18 ambayo nchii imekuwa katika mfumo wa Vyama vingi vya Siasa, kuna vyama vingine ambavyo vimekuwa ni kama debe tupu ambalo haliachi kupiga kelele, akitolea mfano Chama cha Chadema.

Anasema sio CHADEMA, TLP, CUF, NCCR-MAGEUZI ambao wana ubavu wa kumbana na CCM kwa sasa, na wanaojidanganya wajue hawatafanikiwa labda baada ya miaka 2000 ijayo tena labda endapo watabadili sera zao mbovu.
Anasema chini ya uenyekiti wake, CCM Kilimanjaro, imejipanga kujibu propaganda zinazotolewa na mahasimu wa CCM, viongozi wake na wanachama na kusisitiza kwamba kazi hiyo itafanyika kwa ufasaha, kwa wakati na kwa usahihi tena katika maeneo stahili.
Akiendelea kuanisha baadhi ya kazi muhimu na maeneo ambayo uongozi wake unadhamiria kufanyia kazi mwenyekiti huyo anasema, kwa saas kazi kubwa ni kuhakikisha CCM, kinajiendesha chenyewe na amejipanga kuendeleza miradi na vyanzo vya mapato vilivyopo na vitakavyoibuliwa kwa kutumia wataalamu wa fani husika.

Pia, anazungumzia swala la kuthamini nguvu na uwezo wa wanachama, hasa viongozi na kusisitiza katika uongozi wake hakutakuwa na taratibu wa kuchaguana kwa kutazama sura, kabila wala ukoo.

“Tumejipanga kujiimarisha kwa kuteua na kuchagua watu madhubuti, sahihi, lengo letu likiwa ni kuunda safu madhubuti ya uongozi na katika utaratibu huo hata wanachama tutahakikisha wanakuwa watu sahihi na sio kuwa na idadi kubwa ya watu wasiokuwa na mapenzi na chama.

Mwenyekiti huyo wa CCM mkoa wa Kilimanjaro, alizaliwa mwaka 1954 na kuchukua stashahada ya juu katika kazi ya Jamii-NSWTI (1982- 1985), utawala, menejimenti,sheria za kazi mwasiiano na Menejimenti-London 2004 pamoja na mafunzo ya nje ya nchi- Mauritius 2002.

WASIFU WAKE

Alifanya kazi katika kiwanda cha Sukari TPC kama meneja Rasilimali kabla ya kustaafu kwa hiari 2009akiwa katika nafasi ya kiongozi mwandamizi.

Mwenyekiti huyo amewahi kupata nafasi ya kiongozi ndani ya CCM, ambapo mwaka 1986-1989 alifanikiwa kuwa mjumbe wa kamati ya siasa Tawi la CCM kiwandani, mjumbe wa kamati ya siasa tawi la langasani, Arusha chini, mwaka 2001-2005, Mwenyekiti wa CCM kata ya Majengo, manispaa ya Moshi mwaka 2012, Oktoba 18 2012 akachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kilimanjaro, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM Taifa, Mjumbe wa Kamati ya  Siasa ya CCM mkoa wa Kilimanjaro na Mjumbe wa mkutano mkuu CCM mkoa wa Kilimanjaro.


0756038214/0654724337

MWISHOmsaada wa:http://kijiwechetu.blogspot.com

No comments:

Post a Comment