Pages

Pages

Tuesday, November 13, 2012

Totoo Ze Bingwa aibukia Wazee wa Ngwasuma

Totoo za Bingwa 

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
REPA wa zamani wa bendi ya Akudo Impact, Totoo ze Bingwa, mwishoni mwa waki alifanya vitu adimu katika shoo ya bendi ya FM Academia, maarufu kama Wazee wa Ngwasuma, alipowatembelea wanamuziki na mashabiki wao katika Ukumbi wa New Msasani Club, Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Totoo ze Bingwa aliacha kazi Akudo Impact na kufanya kazi kivyake, juzi alipanda jukwaa la Wazee wa Ngwasuma na kufanya makubwa, akikumbukia ukamuaji wake wa zamani, zikiwapo rapu zake zinazotikisa katika kona ya muziki wa dansi.

Repa huyo aliingia ukumbini hapo akiwa kama shabiki wa muziki wa dansi, hadi pale alipooshikwa na mzuka na kuamua kujipeleka jukwaani kwa ajili ya kuwaimbia mashabiki wa bendi ya FM Academia, maarufu kama Wazee wa Ngwasuma.

Hata hivyo huo ni utaratibu mgumu kwa Ngwasuma kufanywa, maana mara kadhaa wamekuwa wakiwawekea ngumu wasanii kupanda jukwaani kwa ajili ya kulinda heshima ya shoo yao inayoingiza mashabiki lukuki katika kumbi zao.

Shoo ya juzi katika ukumbi huo ni mwendelezo wa matukio ya kiburudani yanayofanywa na wanamuziki wakali wa bendi hiyo, wakiongozwa na Rais wa Vijana, Nyosh El Sadaat, akiwa sambamba na Patchou Mwamba.

Nyimbo ambazo zimekuwa zikipendwa na wadau na mashabiki wao ni pamoja na Otilia, Vuta Nikuvute, Anna na nyingine zinazowapa raha wahudhuriaji wa shoo zao.

Akizungumzia shoo hiyo, Nyosh alisema kwamba bendi yao ipo imara na malengo ya kufanya vyema katika tasnia ya muziki wa dansi hapa nchini.

“Tupo imara na mipango ya kuendelea kufanya makubwa katika kona ya muziki wa dansi nchini, hivyo mashabiki wetu watuunge mkono kwa namna moja ama nyingine, ukizingatia kwamba tuna wanamuziki wazuri na wajuzi wa kweli,” alisema Nyosh.

Ngwasuma ni miongoni mwa bendi zenye wapenzi wengi hapa nchini kutokana na uimara wake katika uimbaji na utunzi kutoka kwa wanamuziki wenye uwezo wa hali ya juu, akiwamo Nyosh na wengineo wanaounda FM Academia.

No comments:

Post a Comment