Pages

Pages

Thursday, October 11, 2012

Chaguzi za ndani zikibebe Chama Cha Mapinduzi








MGODI UNAOTEMBEA





Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KATIKA mikoa mbalimbali ya Tanzania, kumekuwa kukiendelea na chaguzi za ndani za Chama cha Mapinduzi CCM na kushuhudia majina kadhaa yakigonga vichwa vya watu wengi.

Chaguzi hizo zimeanza siku chache baada ya Mwenyekiti wake, Jakaya Mrisho Kikwete, kuwapasha wabaya wao kuwa chama hicho hakiwezi kufa, hasa kwa wanachama wao kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi mbalimbali za chama hicho.

                                          Jakaya Kikwete, Mwenyekiti wa CCM


Nafasi kama vile Mwenyekiti wa Mkoa, Wilaya, Katibu, Mweka Hazina katika ngazi mbalimbali, pamoja na Mjumbe wa NEC Taifa.

Hizi ni nafasi zilizoombwa kwa wingi mno na kuonyesha jinsi chama hicho kinavyoendelea kuungwa mkono na wanachama wengi, ingawa baadhi ya wapinzani wanaona chama hakina mashiko na kinajichimbia kaburi.

Ni matokeo mazuri mno. Kila mtu anayapenda kwa wale wenye mapenzi mema na chama chao kinachojiweka katika umahiri wa aina yake na kushindana na vyama vinavyoendelea kuzaliwa kila siku na kuungwa mkono na watu wake.

Kama idadi ya watu walioomba kuteuliwa kugombea nafasi hizo zimeongezeka, kwanini waseme chama kimekufa?

Hata hivyo wahenga walisema lisemwalo lipo. Na katika kuwasikiliza wadau hao, lazima ukweli usemwe na juhudi ziwekwe kama tahadhari ya kukijenga chama.  Je, chaguzi hizo za ndani zina manufaa na chama?

Je, wale walioenguliwa katika nafafsi hizo wamekubali matokeo au ndio wanaanza kujenga matawi yao kwa ajili ya kukihujumu chama chao? Vipi wale walioshindwa katika chaguzi hizo, je wamekuabali kuwa hayo ni matokeo ya kawaida?

Hili linapaswa kueleweka vizuri. Leo wenye chama chao wanaweza kufurahia kuwa chama bado kinapendwa, lakini wachache wao wakawa tofauti. Kwa mfano, Waziri Mkuu wa zamani, Fredrick Sumaye ameshindwa nafasi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), kupitia Wilaya ya Hanang, Mkoa wa Manyara.

Sumaye ameshindwa mbele ya mwanasiasa mwenzake wa CCM, Dk. Mary Nagu, ambaye pia Mbunge wa Jimbo la Hanang na Waziri wa Nchi, Ofisi wa Rais, Uwekezaji na Uwezeshaji.

Uchaguzi huo ni kati ya ile inayochanganya vichwa vya watu wengi, ukizingatia kwamba chaguzi za ndani za CCM zimekuwa na matokeo magumu na joto la ushindani kwa kila mgombea na yule anayepiga kura.

Haijulikani kwanini chaguzi za chama hicho ni ngumu. Labda ni kwasababu wanaopiga kura ni wenye kufanana itikadi, ingawa kwenye malengo hutofautiana kwa kiasi kikubwa.

Kujuana au kurubuniwa kwa rushwa nako ni hatua ngumu kwa chama chao. Ingawa rushwa hukumewa na kila mtu, lakini sio sababu ya kuamini kuwa kichocheo hicho ndani ya chaguzi kimeachwa.

Kikwete alitahadharisha kuwa yoyote atakayebainika anatoa rushwa kwenye uchaguzi huo, hatachekewa, akiwa na maana ya wagombea wote kuacha kutumia rushwa.

Wakati Kikwete anasema hivi, wale wagombea na wapiga kura wao wanapaswa kuwa na uzalendo na chama chao. Wao wasipokuwa makini, uwepo wao hauwezi kuwa na manufaa zaidi ya kukibomoa chama chao.

Wafanye siasa zenye mashiko na mvuto kwa kila mmoja wetu. Wawe kioo cha jamii ndani ya chama au nje ya chama. Wasifanye siasa za kujionyesha mbele ya hadhira, huku malengo halisi, yakiwamo kutetea maslahi ya chama yakiwa adimu.

Kila mgombea au kiongozi wa chama lazima avae uhusika na kukitetea chama chake mbele ya wapiga porojo wengine, hasa waliokuwa upande wa upinzani.

Kama Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kinahaha kufanya mikutano yao mikoani kujenga chama chao, kwanini hawa wa CCM wakae hadi Uchaguzi Mkuu.

Chadema wanatamba na kauli mbiu zao, Dira ya Mabadiliko Movement for Change (M4C), wakati Chama cha Wananchi (CUF) wamekuja na kauli mbiu yao ya (Vision for Change) (V4C), tena wakianzia harakati zao hizo katika ngome ya Chadema, jijini Arusha.

Baada ya kuibuka hayo, Chadema na CUF walianza kurushiana makombora wakisema kuwa chama hicho kimedandia hoja na mwelekeo wao, ingawa CUF nao baadaye walijibu kwa kusema wao ndio waasisi wakubwa.

Kwa mujibu wa CUF, mwaka 2008 na kuiweka rasmi kwenye ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010, hivyo yoyote anayefikiri kuwa hoja yao imetoka Chadema wanajidanganya.

Sitaki kusema nani mkweli kati ya Chadema na CUF, ila hizo ni changamoto nzuri za siasa za Tanzania, zinazoongozwa na CCM iliyokaa madarakani kwa miaka mingi, tangu Taifa hili lilipopata Uhuru wake mwaka 1961.

CCM wala isisononeshwe na vuguvugu la mabadiliko kwa Chadema na CUF, au hata vyama vingine navyo vikifuata nyayo hizo kwa ajili ya kuwapatia elimu ya uraia Watanzania na kuleta ushindani katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka 2015.

Kikubwa kinachotakiwa kufanywa na hao wana CCM ni kukubali kujifunza kutokana na makosa, sambamba na lengo la kuendelea kukaa madarakani kwa kufanyia kazi kero za Watanzania.

Kwa siku za hivi karibuni, Serikali inayoongozwa na CCM, chini ya Kikwete, imekuwa ikifanyia kazi kero hizo, zikiwamo za usafiri, jambo linalowafanya watu waanze kuamini huenda mambo yakawa mazuri katika siku za usoni.

Haya yakiendelezwa na kubuniwa  miradi mingine ya maendeleo, watu wataichukia CCM kwa mambo mengine, likiwamo hilo la ukongwe wake.

Katika kulijua hilo, ni jukumu la kila kiongozi wa CCM, kijana au mzee, mwanamke au mwanaume kufanya kazi kwa ajili ya chama chake.

Najua mapungufu kwa baadhi ya waliochaguliwa au kupitishwa kuwania nafasi hizo haziwezi kukosekana, lakini kama wenyewe wanajua hilo wanaweza kuyafanyia kazi, ndio maana kamati ziliona wanafaa wagombee nafasi hizo.

Watu kama vile Amos Makalla, Juma Nkamia, Mwita Gachuma na wengineo ni kati ya wale waliofanikiwa kushinda katika nafasi walizoomba mwaka huu.

Makalla ambaye pia ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, ameshinda Mjumbe wa NEC Taifa, kupitia Wilaya ya Mvomero, wakati Nkamia, ameshinda kwa Wilaya ya Nchemba.

Ukiangalia kwa haraka, utagundua kuwa wanachama wengi na wenye majina makubwa wameshindwa katika chaguzi hizo, hivyo wasipokuwa na moyo wa subira, wataongeza idadi ya makundi hasimu ndani ya CCM.

Kila mmoja akisema aumizwe na kuanguka kwake, hali ya mambo ndani ya CCM itakuwa tete, hivyo kukipasua zaidi katika uchaguzi Mkuu ujao. Hakuna anayebisha kuwa waliochaguliwa leo, ndio watakaoibeba au kukiangusha chama mwaka 2015.

Wakifanya siasa zenye tija na malengo ya dhati, sidhani kama chama kitaanguka, hasa kama wakikubali matokeo na kuwabeba kila anayetajwa na chama, iwe kwenye nafasi ya Urais, Ubunge, Udiwani au Uenyekiti wa Serikali za Mitaa.

Najua yapo machungu makubwa ya kuachwa au kushindwa bila sababu za msingi, lakini ifikie wakati wanachama wote wawe kitu kimoja. Kwa mujibu wa Kikwete, sio kila mmoja wao anaweza kuwa kiongozi ndani ya CCM.

Walioachwa au watakaoshindwa katika chaguzi zinazoendelea ndani ya chama, wote wawe kitu kimoja na kuleta ushirikiano kwa ajili ya kukiweka chama chao katika mazingra mazuri ya ushindi na kuonyesha kuwa bado wanakubalika.

Haya yatatimia kama wote wakiwa kitu kimoja na kuacha zile siasa za kupakana matope, kutukanana au kurushiana makombora yasiyokuwa na msingi wowote. Kunyukana kwao, ni hasara kwa chama chao na kuvipa kiburi cha majigambo vyama vya upinzani vinavyotembea kwa matao kwa kuona uwezo wa kufanya lolote kwa Watanzania wanao.

Vyama ambavyo vimekuzwa na Serikali ya CCM, vinavyokula ruzuku za Watanzania, huku vikiwa na jeuri kubwa au uchu wa kushika dola, ingawa katika harakati zao hizo, wanaweka mbele maslahi yao na kuacha moyo wa uzalendo nyuma, hali inayoweza kuleta vurugu kubwa kama kila mmoja atakuwa na uchu wa kushika dola.

Huo ndio ukweli. Kila mmoja wetu aujuwe na kuufanyia kazi, wakiwamo washindi au washindwa katika chaguzi za ndani za CCM zinazoendelea kutimua vumbi katika mikoa mbalimbali ya Tanzania na kuleta vicheko na vilio kwa wenye nia ya kuwa viongozi wa chama hicho, kama mwanzo wa kuweka dira ya kushika nafasi kubwa zaidi iwe kwenye chama au serikali.

0712 053949
0753 806087

Mwisho


No comments:

Post a Comment