Pages

Pages

Friday, September 21, 2012

Fiesta ilivyowapagawisha Dodoma na Morogoro




                          FIESTA 2012 DODOMA NA MOROGORO

                                                       AT akiwajibika jukwaani
                                               Linah Sanga, akifanya mambo
                                          Shetta akifanya mambo jukwaaani.
 
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MASHABIKI wa muziki wa mkoani Dodoma, Septemba 14, walipata burudani za aina yake katika Uwanja wa Jamhuri, lilipofanyika tamasha la Fiesta 2012, lilioanza kutimua vumbi mapema mwezi uliopita, mkoani Kilimanjaro.

Mbali na Dodoma, tamasha hilo pia liliendelea katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, Jumapili ya Septemba 16, huku mashabiki wao wakibaki na hara mtindo mmoja kutokana na tamasha hilo.

Wasanii ambao walitoa burudani katika tamasha la Dodoma na Morogoro ni pamoja na Recho, Dayna, Linah, Mwana FA, Godzilla, Shetta, Stamina, AT, Juma Nature, Diamond, Rich Mavoco na Ben Pol.

Mbali na wasanii hao wanaokubalika hapa nchini, pia wasanii wachanga kama kawaida walianza kutoa burudani katika uwanja huo wa Jamhuri Dodoma, ikiwa ni utangulizi wa tamasha hilo na kiu ya kuibua wasanii wapya.

Burudani hizo zilianza jioni kwa wasanii wachanga kupanda jukwaani kutangaza vipaji vyao katika tamasha linaloingiza watu wengi kwa wakati mmoja, jambo ambalo linasababisha uwanja kujaa pande zote.

Kila msanii mchanga wa Morogoro na Dodoma, walikuwa na shauku ya kufanya vyema kwa kuimba nyimbo moja nzuri, ikiwa ni dalili njema ya kutangaza cheche zao kwa wadau wao katika uwanja huo.

Mara baada ya kumaliza kwa taratibu za burudani za wasanii wachanga, moto ulianza kwa kuwapa nafasi washindi watatu wa Super Nyota, wakiongozwa na Young Killer, mwimbaji mdogo mwenye makali ya kutisha.

Wasanii hao wamewekwa katika tamasha hilo kama sehemu ya kuonyesha cheche zao, baada ya kupatikana katika shindano la kusaka vipaji, ikiwa pia ni utangulizi wa ufunguzi wa tamasha hilo la Fiesta.

Baada ya kumaliza kwa wasanii hao watatu wa Super Nyota, msanii aliyeibukia mkoani Morogoro na wimbo wake ‘Mafungu ya Nyanya’, Mwanaisha Said, maarufu kwa jina la ‘Dayna’ alipanda jukwaani akifanya vitu vya aina yake.

Dayna kwanza aliwatanguliza madansa wake walioingia jukwaani kwa mbwembwe za aina yake, wakicheza na kujipanga kishujaa na kupandisha Bendera ya Taifa ya Tanzania, wakifuatiwa na kupiga wimbo wa Taifa.

Wakati wanakatisha kuimba wimbo huo, Dayna alipanda jukwaani, akisababisha shangwe kwa mashabiki wengi uwanjani hapo, wakifurahia alivyojipanga katika shoo yake kwenye tamasha hilo.

Alipomaliza kuimba nyimbo zake, ukiwamo ule wa Mafungu ya Nyanya, Nivute Kwako na nyinginezo, mwanadada huyo alishuka na kupanda jukwaani kwa msichana kutoka Tanzania House of Talents (THT), Reyker, akifuatiwa na Rehema Sundi pamoja na Recho, anayetamba na wimbo wake wa Kizunguzungu, Upepo na huu wa Nashukuru Umerudi unaofanya vizuri kwa sasa.

Recho anatamba katika chati za muziki kutokana na umahiri wake wa kushambulia jukwaa, huku akitokea kwenye taasisi hiyo ya kulea na kukuza muziki ya THT, iliyoibua wasanii wengi wenye uwezo wa kutisha.

Mara baada ya mwanadada huyo kumaliza kuimba, alimuachia Ommy Dimpozi kuendelea kushusha burudani. Hata hivyo, Ommy ni kama alipanda kwa mkosi, maana umeme ulisumbua kwa dakika kadhaa.

Cha kushangaza ni kwamba, licha ya umeme kusumbua uwanjani hapo kwa dakika kadhaa, lakini Ommy aliendelea kushangiliwa na wadau kuimba kama kawaida, hivyo kuonyesha kuwa msanii huyo anakubalika kupita kiasi.

Kitendo cha kumaliza kuimba kwa mkali huyo aliyeacha historia mkoani Dodoma, alipanda jukwaani Rich Mavoco, akifuatiwa na Stamina, msanii aliyetingisha uwanja mzima kwenye shoo hiyo.

Wasanii wengine waliofuata kutoa burudani katika tamasha hilo ni Shetta, Ben Pol, Linah, Mwana FA, aliyesindikizwa na AY, ambaye hata hivyo hakuwa kwenye ratiba ya kupanda jukwaani kutoa burudani.

Msanii ambaye pia atakumbukwa ni AT aliyepanda jukwaani mara baada ya kushuka wakali wa Hip Hop na R&B Ben Poli, yeye alipanda jukwaani na kuwashawishi mashabiki wamsikilize na kucheza nyimbo zake.

Wengi katika shoo kubwa kama hizo hushindwa kuwafanya watu wacheze, hasa hawa wa mduara kama AT, anayetokea mjini Zanzibar.

Shoo ya Dodoma ilimalizwa na Juma Nature usiku wa manane, baada ya kumaliza wakali wote, akiwamo Godzilla, mkali mwenye maskani yake mitaa ya Salasala.

Utaratibu kama huo ulionekana pia katika mji wa Morogoro, ambapo mashabiki wengi walionekana kupagawa kabla ya shoo hiyo wakiwachekea wasanii na kujipanga kwa ajili ya kuingia kwenye shoo hiyo.

Hata hivyo, mashabiki walipoingia kwenye uwanja huo wa Jamhuri mjini Morogoro, walikuwa wazito sana kucheza na kupagawa kama ilivyokuwa kwa wakazi na mashabiki wa mkoani Dodoma.

Fiesta inaandaaliwa na Kampuni ya Prime Time Promotion pamoja na Clouds Media Group, likifanyika kila mwaka. Kwa mwaka huu, Fiesta ilianza kutimua vumbi katika mji wa Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Katika kila mkoa wanapofanya shoo hiyo, kunatanguliwa na kazi za kijamii, ikiwamo kutembelea vituo vya watoto yatima na kuwapa misaada ya aina mbalimbali pamoja na kupata fursa ya kubadilishana nao mawazo.

Kwa mkoa wa Dodoma, wasanii na waandaaji wa tamasha hilo walitembelea kituo cha watoto yatima kinachojulikana kama Kijiji Cha Matumaini, kilichoanzishwa rasmi mwaka 2002.

Usiku wa shoo hiyo ulifunguliwa na Mkuu wa Mkoa, Rehema Nchimbi, wakati ile ya Morogoro ilihudhuliwa pia na Mkuu wa Mkoa wake, Joel Bendera, ambapo pia wakuu hao husisitiza suala la amani kwa tamasha hilo.

Mikoa iliyofuata kwa burudani hiyo ni pamoja na Tanga, Musoma mkoani Mara, Shinyanga, Mwanza, Dodoma, Morogoro, huku wiki hii likipangwa kufanyika jana Ijumaa katika mkoa wa Mbeya, wakati kesho Jumapili tamasha hilo pia litafanyika mkoani Iringa, Uwanja wa Samora.

0712 053949
0753 806087

Mwisho

No comments:

Post a Comment