Pages

Pages

Thursday, October 20, 2011

Serikali ipige jicho lake BASATA

KUJADILI vitu vya maendeleo kwa Tanzania kunahitaji moyo wa chuma kama alivyowahi kusema muasisi wa Taifa hili, Hayati, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere juu ya masuala nyeti ya Azimio la Arusha.

                                                        Dayna Nyange, msanii

Mwalimu, mmoja wa viongozi wanaopendwa barani Afrika, Oktoba 14, ilikuwa ni kumbukumbu ya kifo chake, baada ya kumaliza siku zake za kuishi duniani, akitumika kama mkombozi kwa Taifa hili, linaloongozwa na Rais wake, Jakaya Mrisho Kikwete.
 
Nasema moyo wa chuma, maana hata kama uwe mjuzi wa kujadili mambo hayo kwa kiasi gani, hao wanaojadiliwa kubadilika kwao ni kazi ngumu. Katu hawataki kusikia au kuona yale wanayofanya kwa faida ya nchi yao .
 
Hata hivyo, sio jambo la busara kubaki kimya. Taifa linazidi kutumbukia kwenye shimo baya la umasikini na wachache wao wakizidi kuneemeka. Utajiri ni wa kwao, wakati wenzao wanazidi kuwa masikini wa kutupwa.
 
Tanzania ya leo, ni kazi ngumu kupata ajira kama huna fedha. Suala kama hilo , linaonyesha ni jinsi gani mambo yanavyotakiwa kubadilika kwa faida ya wananchi wake. Tuache hayo turudi kwenye lengo la makala haya.
 
Wakati Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo akiteua safu mpya ya uongozi ya baraza la Michezo Tanzania , nadhani ipo haja pia ya kuangalia upya mwenendo wa uongozi wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).
 
Baraza hili muhimu kwa Tanzania naweza kusema limekufa. Viongozi wake wengi hawaonyeshi jitihada zao za dhati kwa maendeleo ya sanaa ya Tanzania . Wasanii waliokuwapo bado kazi zao hazina jipya, huku wengineo tungo zao zikikosa sifa.
 
Ni hao wanaoacha kutunga nyimbo za kukosoa madawa ya kulevya, kubweteka majumbani au kwenye vijiwe vya kahawa, huzama zaidi kwenye tungo za kidunia. Hapa lazima niwe muwazi na bila ya kuweka woga wowote kwa ajili ya Tanzania .
 
Sitaki kusema viongozi wa BASATA wote wameshindwa kazi, ila Serikali lazima iwapige jicho ama kuwaelekeza vitu vizuri kwa ajili ya maendeleo ya Taifa. Nimepata nafasi ya kuchunguza utendaji kazi wa BASATA na kubaki mdomo wazi.
 
Mengi wanayofanya, si maendeleo kwa sanaa ya Tanzania . Uchunguzi wangu unaonyesha kila msanii wa nje anayekuja hapa nchini hutakiwa alipe fedha nyingi kama gharama za kuja kufanya kazi Tanzania , zisizopungua milioni moja.
 
Kwa mfano, wapo wanaotozwa hadi kiasi cha shilingi miliona moja, huku wakitakiwa walipe fedha za faini, kama mtu huyo ameanza kutoa habari kwa wanahabari kwa ajili ya kuwajulisha Watanzania.
 
Sawa, ila wakati mwingine wadau hao huonewa kwa makosa ambayo sio yao . Nasema hivyo huku nikiangalia upekuzi wa waandishi kujua habari hata zile wasizotakiwa wazifahamu kwa wakati huo.
 
Pamoja na hayo, kama ndivyo hivyo, fedha hizo za faini kiasi cha milioni moja hupelekwa wapi? Je, nchi hii inafanya juhudi gani kutangaza sanaa ya Tanzania ? Wasanii wetu wa ndani wanafanyiwa vitu gani kwa mafanikio yao ?
 
Msanii wa ndani kubaki kuimba peke yake ni jambo linaloweza kuangamiza kipaji chake. Inatakiwa apate ushindani, ama kusoma kutoka kwa wenzake. Hivyo basi, kitendo cha BASATA wao kujifanyia mambo kienyeji ni kuharibu mfumo mzima wa sanaa.
 
BASATA wao huku wakiweka mbele fedha, lazima utendaji kazi wao uwe mzuri, maana uliopo sasa ni kubuluzana na uliojaa maslahi binafsi. BASATA iliyopo sasa ni kuwakomoa wadau wenye uwezo wa kukuza sanaa kwa manufaa yao .
 
Sitaki nionekane tofauti juu ya hili, ndio maana hapo mwanzo wa makala haya nikatahadharisha maana wanaopewa ukweli hupayuka wakisema wanayojua wenyewe. Inatia aibu, kama kila mtu anahifanyia anavyojua mwenyewe.
 
Huku wadau tukipigania utendaji mbovu wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), bado kuna vitengo nyeti vinaachwa tu bila kukosolewa. Nisema tu, nitakuwa mkweli kusema kila ninalojua kwa maendeleo ya Taifa langu, hata kama nitachukuliwa tofauti.
 
Kuna mambo mabaya mno yasiyofaa kufanywa na viongozi wetu, iwe ni kwenye michezo ama sanaa inayofaa kuheshimiwa Dunia nzima. Angalia Barani Ulaya, wengi wanafanikiwa. Muangalie mwanadada Rihannah, Jay Z na mke wake Beyonce, utakubali kuwa sanaa inalipa.
 
Sio huyo tu, bado wapo wakali wengine wanaovuna fedha lukuki, kutokana na kukuta mfumo mzuri katika nchi zao, ikiwamo hakimiliki. Siamini kama wasanii wetu wa ndani wataendelea kuachwa tu, hali ya kuwa wana utajiri wa vipaji.
 
Ni wakati wao Serikali kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuangalia upya sera zao na sera za mabaraza yake, likiwamo hilo la BASATA. Sioni juhudi na harakati za kukuza sanaa ya Tanzania zaidi ya kuidumaza.
 
Je, ni wasanii wote wanatakiwa walipe fedha hizo zikiwamo faini au ni wachache? Ushahidi unaonyesha kuwa, kama ni kweli, basi BASATA wanavuna fedha nyingi, maana wengi wanakiuka masharti hayo. Yani kupata kibali, kabla ya kuvuja kwa ujio wao.
 
Hivi kweli, mwandishi kuandika ujio wa msanii fulani ni kitendo kibaya kiasi cha kuwafanya BASATA walazimike kutoza faini hizo? Jamani, kwanini Tanzania tunakwenda ovyo namna hiyo?
 
Kwanini tamaa ya kujaza matumbo yetu ipo mbele kuliko kusudio la kweli la kuwakomboa Watanzania kwenye vita hii ngumu ya maradhi, ujinga na umasikini? Sikatai, msanii alipe gharama za kuishi nchini, ila nyingine ni wizi tu.
 
BASATA unaweza kufuatilia kibali kwa muda mrefu bila hata kukupatia. Nia yao ni mdau huyo avunje amri yao ya kuzungumzia ujio huo hata kwa marafiki zake, ili wapate hiyo shilingi laki tano au milioni moja.
 
Yuko wapi Emmanuel Nchimbi, waziri wa Wizara hiyo? Hivi kweli ndivyo BASATA wanavyotakiwa wajiendeshe? Sina nia mbaya, ila kusudio ni kujiendesha vema kwa manufaa ya Tanzania na sio kwenda ndivyo sivyo.
 
BASATA wanatakiwa wasome alama za nyakati. Wanatakiwa wawe na fikra pevu juu ya sanaa ya Tanzania , inayozidi kuyumba. Wengi kazi zao ni mbaya na zinakosa maudhui na maana halisi ya sanaa ya Tanzania , hata kwenye matamshi.
 
Bado sanaa nyingine zinakosa mwamko, ikiwamo ya nyimbo za asili, zile za makabila tofauti, zilizokuwa zikivuma wakati huo. Sanaa kama ususi, uchongaji, uchoraji sasa zimeadimika kabisa katika Taifa hili.
 
Wanaotamba ni Bongo Fleva, tena kwa kazi ambazo nyepesi, zimekosa soko na mvuto linapokuja soko la Kimataifa. Wengi wao mavazi yao ni karaha tupu. Bado wabunifu ni mavazi wapo wapo tu. Ukienda nchi za wenzetu wamefanikiwa, kiasi cha sasa kuangalia mazuri yao .
 
Sisi tuna wasanii wengi tu, lakini bado Makhirikhiri wamekuja kuteka soko la Tanzania, bila kusahau ndugu zao Dikakapa Traditional Dance, ambao hadi sasa wapo mikoani huko wakitangaza muziki wao wa asili.
 
Sawa, waje tu, maana najua ni somo kwa wadau, viongozi na wasanii wa ndani. Lakini kuwekewa ngumu, au wadau kutozwa fedha nyingi ni kuwadhulumu wao na kuibananga sanaa ya Tanzania , inayotakiwa itangazwe na kila mmoja wetu.
 
Kiu yangu ni kuona sanaa inapiga hatua kwa kuwa na viongozi wenye uelewa, mipango na uthubutu katika kazi zao, sio wale wanaotamani zaidi kumiliki vitu vya thamani katika utawala wao, huku wanavyoviongoza vikijikongoja.
 
Ndio maana naitaka Serikali, kuangalia zaidi mfumo mzima wa BASATA na ndugu zao COSOTA, maana ni muhimu na wameshika funguo za mafanikio kisanaa ya wasanii wa Tanzania , wanaoshi kama njiwa, kula chini kulala juu.
 
Naomba kutoa hoja waungwana
0712 053949
0753 806087

No comments:

Post a Comment