Pages

Pages

Monday, September 26, 2011

Waandishi wa habari za michezo wamegeuzwa kandambili










Waandishi wa habari juu na Ofisa Habari wa TFF Boniface Wambura picha ya chini.



NIMEKUWA karibu kufuatilia sakata la waandishi wa habari za michezo, Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo TASWA na Shirikisho la Soka nchini (TFF), ambao wote kwa pamoja wanatakiwa wafanye kazi zao kwa ushirikiano mkubwa.

Mengi nayaona na kuyaacha yapite. Mengine yananichekesha mara baada ya kusumbua akili yangu kwa dakika kadhaa kuyachambua kadri ninavyoona inafaa. Hata hivyo, katika hili la waandishi wa habari za michezo kugeuzwa kandambili, siwezi kuvumilia.

Nasema hivyo kwasababu mchango wa waandishi wa habari unajulikana na wanatakiwa waheshimiwe kwa namna moja ama nyingine. Takribani mwaka mmoja sasa, watu hawa wameendelea kunyanyasika.

Mara kadha wanajituma kupita kiasi kuwahabarisha wadau wa michezo, hata hivyo mwisho wa siku wanachoambulia ni matusi ya reja reja. Utawakuta wakishinda kutwa nzima katika ofisi za Shirikisho la Soka nchini (TFF), wakisubiri vitambulisho vya kuingia uwanjani.

Hiyo huja katika mechi za Kimataifa, ambazo kabla ya mechi hizo, vyombo vya habari na waandishi wao hufanya juhudi kubwa kutoa habari kwa wadau na mashabiki na kuingia kwa wingi uwanjani, kitu kinachowafanya waingize fedha nyingi.

Hapa lazima tufanye jambo. Maana hali hii ikiendelea, waandishi wa habari za michezo wataendelea kuwa kandambili, kuogewa na baadaye kuachwa nje.

Mbaya zaidi, juhudi zinazofanywa haziwezi kuokoa thamani yao. Mchango wao ni mkubwa mno. Hawa hawastahili kunyanyasika. Waandishi hawa wanaosifiwa kila siku kwa kazi zao, waliwahi kuachwa katika kivuko kwa sababu nilizoshindwa kuzielewa.

Mengi yalizungumzwa. TFF yenyewe ilisema waandishi wa habari baadhi yao, walitoa maneno ya kashfa zilizowachukiza wahusika. Sawa, huwenda ni kweli. Ila, nani alistahili kulipa gharama za kivuko, ni waandishi wenyewe au TFF waliowaita?

Kwanini utaratibu wa kuingilia uwanjani ubadilishwe? Je, zile zilizokuwa zikitumika kabla yao, wakati Fredrick Mwakalebela ndio Katibu Mkuu, ni mbaya? Kwa mujibu wa takwimu zilizofika TFF na TASWA, waandishi jumla ya 170 waliombewa vitambulisho vya kuingilia uwanjani.

Kwanini mpaka sasa havijatoka? Ukiangalia kwa jinsi vyombo vya habari vilivyokuwa vingi ni idadi ndogo mno. Nasema hivyo kwasababu wanachoandika ni thamani na matangazo ya bure kwa TFF.

Kama wangepaswa walipe kama matangazo kwa kila kinachoandikwa na magazeti, redio au televisheni, ni dhahiri fedha hizo hawana uwezo wa kulipa? Kama waandishi wamechangia kuingia mamilioni ya shilingi, kuna ubaya gani waandishi 170 kuingia bure uwanjani, tena sio wote wanaoweza kuhudhulia mechi.

Ngoja niseme ukweli maana najua ndio unaoweza kuokoa ushirikiano unaoelekea mwishoni kwa waandishi wa habari na TFF, japo kuwa najua naweza kujiweka tabuni kwa wale wasiopenda kuambiwa ukweli. Uwanjani kila mtu huwenda kwa kazi yake. Wengine huwenda uwanjani kwa ajili ya kuandika makala na mengineyo.

Wengine huingia kwa ajili ya kuripoti mechi. Hugawana majukumu. Hakika hali ni mbaya mno. TFF wanasema wahariri wasiingie bure uwanjani.

Na kama wakitaka kuingia, vyombo vyao vya habari viwalipie. Jamani, mhariri ni nani na mwandishi ni nani? Ndio  maana nasema suala hili lazima lichukuliwe kipaumbele maana hali inazidi kuwa mbaya? Leo, mambo yanavyozidi kuwa magumu, ushirikiano ni jambo la lazima,

Tamaa ya pesa nyingi zinazotokana na waandishi wa habari zisipoteze thamani yao na kusababisha kususa. Unaweza kushangaa, ila kikweli siwezi kuvumilia. Nawaonea huruma TFF kupitia kwa Rais wao Leodgar Tenga na Katibu Mkuu wake Angetile Osiah.

Muda wao mwingi wanautumia kurushiana maneno na waandishi wa habari 170 waliombewa vitambulisho na kukosa ujuzi na maarifa ya kuendeleza michezo. Timu ya Taifa, Taifa Stars ilishindwa kwenda Sudan huku wao wapo ofisini.

Yanga, Simba wamekuwa watawala wa soka nchini. Wasemalo wao ndio linalofanywa. Wamekaa tu. Wakija kuzungumza ni aina ya kadi chache za waandishi wakitaka wasiingie uwanjani, maana nafasi zitajaa.

Kwanini? Nani amewatuma? Huu ni wizi mtupu na ubabaishaji mkubwa? Osiah ni mwandishi anajua mchango wa ndugu zake hao wasiokuwa na thamani kwa TFF ya leo. Ujinga huu utakwisha lini? Inakuwaje mvutano huo umalize mwaka?

Kwa kila mechi, vyombo vya habari viwalipie waandishi wao 170 kwa tiketi ya elfu 10,000 kila moja ni sawa na shilingi 1,700,000. Vipo vyombo vingi vya habari, lakini magazeti 13 kwa siku yalipiwe Shilingi 1,000,000 ni ndogo ya pesa zilizolipiwa kwa waandishi.

TFF wameangalia suala hili? Mnajua thamani ya matangazo? Kwanini Watanzania mnapenda kupayuka yuka ovyo? Iwapi thamani ya elimu zenu? Mmesomea wapi hadi mkose walau robo ya kuangalia faida na hasara?

Sina nia ya kuwarushia makombora wadau hao na viongozi wa TFF, kwakuwa lengo langu ni zuri. Napenda tujenge nyumba yenye maendeleo.

Tanzania inazidi kufanya vibaya kwenye medani ya Kimataifa. Huu ni muda wa kukaa pamoja kuangalia tatizo lipo wapi na sio kukimbizana na waandishi au kuwagandisha kusuburia kadi zinazobadilishwa kila siku ya Mungu.

Leo hii ligi inaendelea, lakini hutashangaa kuambiwa mwandishi yupo TFF anasubiria kadi na tiketi ya kuingilia uwanjani. Huu ni ujinga. Hii ni aibu yenu na ninasema japo kuwa najua ni vibaya kumsema mtu mkubwa.

Kwanini? Nadhani hapa ipo haja ya waandishi wa habari kuikataa dhambi hii ya kufanywa kandambili, kuwatangazia mechi zao na mwisho wa siku husahau na kukimbilia fedha zinazopatikana kwa mchango wa waandishi.

Ona wakati mwingine uwanja haujai kabisa. Utawaona wamekaa na wadhamini wao, wamewapa viti maalum, lakini wanahabari wamechanganyika na mashabiki. Huyu anarusha chupa, yule amesimama akitoa matusi?

Hawajatengewa sehemu yao ya kukaa na kufanya kazi zao kwa ufanisi. Nadhani hili liangaliwe kwa mapana zaidi.

Chonde chonde TASWA, BMT, TFF na Serikali kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo chini ya Waziri wake, Emmanuel Nchimbi, kuirudisha thamani ya waandishi wa habari za michezo.

Inakera ndio maana siwezi kuvumilia
0712 053949
0753 806087


No comments:

Post a Comment