Pages

Pages

Monday, September 26, 2011

Sanaa ni kazi, wauza sura zindukeni

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
SANAA ni moja ya vitu vyenye mguso mkubwa kitu kinachotakiwa kipewe kipaumbele na wadau wote wakiwamo wasanii wenyewe.
 
Sio kukaa tu na kujipodoa kwa nia ya kupata nafasi zaidi ya kuuza sura, kitu kinachoweza kuharibu mfumo mzima na kiu ya mafanikio kwa wasanii wetu.
 
Kupenda kwangu kuchunguza aina ya maisha ya wasanii wetu, kumenifanya nijuwe mambo mengi kupita kiasi. Wapo wasanii waliovuma miaka ya 2002 lakini sasa hawapo au wapo lakini hawana jipya.
 
Kwa bahati mbaya, hata maisha yao yamekuwa machungu mno kwao. Kuomba sawa wanaweza, ila watamuomba nani wakati walifunga vioo wakati huo wanatoa albamu moja na kupewa gari la Milioni mbili?
 
Hayo ni maswali ninayojiuliza kutwa kucha, ila mwisho wa siku lazima wasanii wenyewe wawe makini. Sanaa ni kazi. Wengi wanaweza kufanikiwa, ila sio kwa kupenda kuuza sura ovyo huku kazi zikiwa mbovu.
 
Sio kuuza sura tu, wakati wanashindwa kufanya mambo yenye tija kwa ajili ya sanaa zao. Kwa bahati mbaya kiloa siku wasanii wanazidi kuongezeka, ila sidhani kama wanazijua athari zinazoweza kuwakumba.
 
Bongo Fleva, ni miongoni mwa sanaa rahisi kufanywa, kitu kinachowafanya vijana wengi waone wana haki na wajibu wa kuitwa wasanii, hata hivyo kasumba yake ni hatari kwa wale wanaojihusisha na sanaa hiyo.
 
Hawafanikiwi kamwe. Maisha yao ni ya kubahatisha, licha ya kuwa kwenye kitu kinachowapa utajiri mkubwa watu wengi duniani.
 
Angalia Barani Ulaya. Wasanii wa kule, waandaaji wa muziki na wengineo wanafanya jeuri ya pesa. Wanashindania fedha, kila mmoja akijiona ni zaidi ya mwenzake.
 
Hapo utashangaa watoto wadogo wanavyoweza kuvuna fedha nyingi kwasababu ya sanaa. Wanaimba kama wanavyoimba wengine.
 
Ila, maisha yao ni ya gharama na yenye mvuto kutokana na kuzaliwa katika nchi zinazopigania maendeleo, maana wanajuwa kuvuma kwa msanii ni dalili njema ya kuvuna utajiri kutoka kwake.
 
Wapo wangapi wanaovuma Marekani? Je, nchi yap imenufaika vipi kwa kukatwa kodi wao, licha ya kuimba wenyewe?
 
Hayo ni maswali tunayotakiwa tujiulize mimi na wewe, maana hakuna haja ya kukesha kwenye kioo kujiremba, wakati hadi jana umeimba bure katika shoo iliyowaingizia watu pesa nyingi na kunufaika na familia zao.
 
Unaona raha kutangazwa? Unaona furaha, maana ndio njia yako ya kujulikana kwa watu kwakuwa huna lengo lingine zaidi ya kuuza sura.
 
Huo ni udhaifu mkubwa na utaendelea kuwakumba wasanii wengi wa Tanzania , maana akili zao hazikuwi. Kila siku ni wale wale.
 
Jamani kwanini mnakuwa hivyo? Hivi hamuoni kufuru za kina Jennifer Lopez, Rihanna, Beyonce na wengineo wana huko wanavyoishi maisha ya gharama.
 
Wao wapo wapo tu. Kama mijisanamu vile. Jamani, sijui Mungu amewaroga Watanzania? Upo uwezekano mkubwa kuwa kasumba hizi kwa wasanii zitaendelea miaka nenda rudi maana hawajitambui.
 
Wasanii wa Tanzania hawana uthubutu. Wameridhika kuwa chanzo cha utajiri wa wenzao, huku wenyewe wakiambulia nafasi ya kuuza sura.
 
Uzeni tu kwa raha zenu, ila hakuna haja yakuingia kwenye sanaa isiyolipa. Ukiacha huko kuuza sura faida gani nyingine wanayopata wasanii wetu, hasa hawa wa Bongo Fleva.
 
Au nao wanataka kuwa wanasiasa kama Mh Joseph Mbilinyi, maarufu kama Mr Two? Sugu huyu ni sawa na ubongo wa Diamond, Mr Blue, Madee, Godzilla na wengineo?
 
Sawa, ila ipo haja ya wasanii wenyewe kujitambua maana huko kuuza sura, bila kuwa na mipango ni sawa na kupoteza muda wao.
 
Watunge nyimbo nzuri zinazovutia bila kusahau kupambana na yote yanayoharibu maisha yao , maana sanaa ni kazi na wale wanaoingia kwa kuuza sura watafute njia nyingine.
 
0712 053949
0753 806087

No comments:

Post a Comment