Pages

Pages

Tuesday, September 27, 2011

Mbunge wa Kilwa amlipua kocha wa Stars

MBUNGE wa Kilwa Kaskazini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Murtaza Mangungu, amemjia juu kocha wa timu ya Taifa, Taifa Stars, Jan Poulsen, akisema kuwa uwezo wake hauridhishi na ipo haja ya kuwekwa pembeni kwa manufaa ya maendeleo ya michezo, hasa mpira wa miguu.

Mangungu ambaye pia ni miongoni mwa wabunge mashuhuri na wanaopenda michezo, alisema hadi sasa tayari kocha huyo ameshashindwa kuiletea maendeleo Tanzania kwa kupitia mpira wa miguu, licha ya kuendelea kukumbatiwa na wadau wachache likiwamo Shirikisho la Soka nchini (TFF).

Akizungumza jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Mangungu alisema ingekuwa nchi nyingine za wenye kuhitaji maendeleo, kocha huyo angeshatimuliwa maana haan jipya na uwezo wake hauridhi.

Alisema kitu kama hicho kinatakiwa kiangaliwe upya na wadau wa michezo, maana hata aina ya upangaji wake wa timu wakati mwingine haina jipya na malengo kwenye medani ya mpira wa miguu.

“Lazima Watanzania tuwe na uthubutu na malengo ya kweli, maana si kila Mzungu anaweza kufundisha soka Tanzania, ndio maana ujio wa Paulsen hauna mpya na ipo haja ya kuwa wakali katika hilo.

“Kama kocha aliyeipa mafanikio Tanzania, Mbrazil, Marcio Maximo amemaliza mkataba wake, kulikuwa na sababu kubwa ya kupatikana mwingine mwenye uelewa na juhudi za dhati kuliko kupeana ajira zinazopoteza fedha nyingi za Watanzania na hakuna cha maana kinachopatikana,” alisema Mangungu.

Stars inajiandaa na mechi yake dhidi ya Morocco, inayotarajiwa kupigwa Oktoba 9, nchini humo, huku malengo ya mashabiki wa Tanzania yakizidi kupotea kutokana na uchezaji mbovu wa wachezaji wake.

No comments:

Post a Comment