https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Friday, November 28, 2014

Migogoro ya ardhi, mipaka ni tishio wilayani Handeni

Na Mwandishi Wetu, Handeni 
SERIKALI Kuu kwa kushirikiana na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya Handeni na Mkoa mzima wa Tanga, wameombwa kuingilia kati mgogoro mzito wa ardhi katika kijiji cha Komsala, wilayani Handeni, ili kuepusha hatari inayoweza kutokea, ikiwamo vita ya wenyewe kwa wenyewe.


Hayo yamesemwa juzi na wananchi wa kijiji hicho katika mkutano ulioandaliwa na taasisi ya Handeni Kwetu Foundation inayofanya ziara katika maeneo mbalimbali, hususan ya wilaya ya Handeni, mkoani Tanga, baada ya kuzinduliwa Mei 8 mwaka huu.


Wakizungumza kwa uchungu mkubwa, wananchi hao walisema kuwa hali ni mbaya, maana kijiji chao kimeendelea kutekwa na kubaki eneo dogo lililoanza kuibua chuki za wazi kwa wananchi.


Mzee aliyejitambulisha kwa jina la Alhaj Ally Yasin Ling’ande, alisema kiuhalisia hakuna kijiji cha Komsala, kwakuwa hawana eneo la ardhi, hasa baada ya wilaya Korogwe kuingia kwenye eneo lao kwa kufikia hata kujenga mnada wa ng’ombe.


“Ukiaangalia usawa palipojengwa mnada, utaamini kuwa hata kwenye shule ya Msingi Komsala pia patakuwa ni eneo la Korogwe, ingawa si sahihi kulinganaa na ramani ya mwaka 1978, jambo linaloonyesha kuwa huu ni mzozo utakaoweza kumwaga damu,” alisema.


Naye William Seif alisema mbali na mipaka hiyo kuwa tata, pia kumekuwa na idadi kubwa ya wageni kumiliki heka zaidi ya 130 na bado wanaingia kwa wenye heka tatu wakiamini kuwa uwezo wao kifedha unawafanya wamudu kesi zinazoendeshwa kwenye mabaraza ya Kata na wao kupata haki.


“Masikini akionewa anakimbilia kwenye Bazara la Kata, lakini huko kumekuwa na danadana nyingi, ukizingatia kuwa siku zote mkono mtupu haulambwi, ndio maana tunaoimba serikali ya wilaya ya Handeni, mkoa na wadau wengine wa ardhi kuja kujionea bomu hili linalosubiriwa kuripuka hapa kwetu,” alisema.


Mwananchi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Bashiri Wabu, alisema kuwa ardhi katika kijiji chao imeuzwa kiholela kwa watu wenye nazo bila kufuata sheria za ardhi, ikiwamo ya kuandaa mkutano wa wananchi wote.


“Kuna watu hawana maeneo kabisa ya kulima, wakati watu wachache wanamiliki maeneo makubwa ambayo hata kuyalima yote hawana uwezo huo, jambo linalokera na kuudhi mno kila tunapoliangalia suala hili katika kijiji chetu,” alisema Wabu, akiungwa mkono pia na Hemed Ngona, Kombo Twaha, wakisisitiza kuwa sheria za ardhi na utawala bora hazifuatwi katika kijiji chao.


Katika mkutano huo ulioanza saa 9 alasiri na kumalizika saa 12 jioni, ulihudhuriwa na watu wengi, huku idadi kubwa ikiegemea katika kero ya ardhi na mipaka.


Aidha Mwenyekiti wa kijiji cha Komsala anayemaliza muda wake, Mwanaidi Said, alisema kero kubwa katika kijiji hicho ni mipaka iliyoshindwa kutatuliwa na viongozi wa juu, licha ya kupeleka malalamiko yao mara kadhaa.


“Kijiji cha Komsala sasa ni kama kitongoji tu, maana kimechotwa katika pembe zote na ndio maana hata wenzetu wa Korogwe wamekuja kujenga mnada wa ng’ombe kwa madai kuwa ni kwao, jambo ambalo hata mwenyekiti atakayefuata litamuumiza kichwa,” alisema na kuwafanya wananchi wapatwe na hofu.


Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo aliyetumia muda huo kuaga wananchi wake, sekeseke la mipaka limeshindwa kutatuliwa, huku akiwataka viongozi kulipa kipaumbele kabla ya matatizo hayajakikumba kijiji chao pale wananchi hao watakapotafuta haki yao.


Naye Msemaji Mkuu wa taasisi hiyo, Kambi Mbwana, aliwashukuru viongozi wa serikali ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni kwa kuwapa ushirikiano, ikiwamo kuruhusu kutembelea katika vijiji mbalimbali kutoa elimu ya uraia na kuhamasisha utawala bora.


“Naomba niwatoe hofu Watanzania wote kuwa mikutano hii ya hadhara hairatibiwi na chama chochote cha siasa, hivyo tunaomba tushirikiane kwa ajili ya kufanikisha maendeleo, hasa kama wananchi watahudhuria mikutano wanapoitwa na viongozi wao,” alisema.


Ziara ya Handeni Kwetu Foundation ilianzia Kata ya Misima, ambapo wananchi wengi wameiunga mkono taasisi hiyo yenye lengo la kuwakomboa wananchi kwa kutoa elimu na kuhamasisha maendeleo ya jamii.





Monday, November 24, 2014

Machenja alipania tamasha la NSSF Handeni Kwetu 2014



Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MSANII wa muziki wa mashairi, Said Machenje, amesema ameanza mazoezi rasmi kwa ajili ya kuhakikisha kuwa anakuwa mmoja wa wasanii watakaotoa burudani kali katika tamasha la NSSF Handeni Kwetu, linalotarajiwa kufanyika katika Desemba 13 mwaka huu, katika Uwanja wa Azimio, mjini Handeni, mkoani Tanga.

Machenje anayeshindana vilivyo na mkali wa muziki huo, Mrisho Mpoto alisema kuwa maandalizi yake yanakwenda sambamba na shauku ya kutembelea kwa mara ya pili wilayani Handeni.

Akizungumzia hilo jijini Dar es Salaam, Machenje alisema kwamba mwaka jana alipanda jukwaani kuimba kwa kushirikiana na kikundi cha Naukala Ndima, ila msimu huu amefanikiwa kupata mwaliko wake binafsi.

Mwimbaji huyo wa 'Kajenge kwa Mumeo' na 'Mila', alisema kwa kualikwa binafsi, kunamfanya apate hamu ya kujiandaa kwa ajili ya kufanya mambo makubwa zaidi ili kuonyesha umahiri wake katika tasnia ya muziki wa mashairi.

“Nashukuru Mungu kwa kupangwa kuwa mmoja wa wasanii watakaotoa burudani katika tamasha la NSSF Handeni Kwetu 2014, wilayani Handeni mkoani Tanga kwakuwa ni mwelekeo mzuri katika maisha yangu ya sanaa.

“Nafanya mazoezi makali kwa ajili ya kujiweka sawa ili nifanye shoo nzuri Desemba 13, katika Uwanja wa Azimio, ukizingatia kuwa nina uzoefu sasa na jukwaa la tamasha hili la aina yake,” alisema.

Wadhamini tamasha hilo ni Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) pamoja na Phed Trans, SmartMind & Partners iliyopo chini ya Anesa Co. Ltd kwa kupitia kitabu cha ‘Ni Wakati wako wa kung’aa, Handeni Kwetu Foundation, Wait & Watch Film Company Ltd, Qs Mhonda J Apex Group of Companies Ltd na Skyblue Security and Risk Mgt Ltd na Michuzi Media Group.





Thursday, November 20, 2014

Wananchi wa Misima, wilayani Handeni, mkoani Tanga waipinga Halmashauri ya Mji

Na Mwandishi Wetu, Handeni

MKUTANO wa kwanza wa taasisi ya Handeni Kwetu Foundation uliyofanyika jana Novemba 19, katika kijiji cha Misima, wilayani Handeni, mkoani Tanga na kuwakutanisha wananchi wote umeibua kero nyingi za wananchi, ikiwamo ya kijiji chao kuingizwa kwenye Halmashauri ya Mji bila ridhaa yao.

Mmoja wa wakazi na wananchi wa kijiji cha Misima, akilalamikia eneo lao kuingia kwenye Halmashauri ya Mji kinyume cha sheria ya utawala bora, ikiwa ni pamoja na kutoshirikishwa kwa lolote na viongozi wa juu.
Taasisi hiyo ilianzishwa mapema mwaka huu na kuzinduliwa Mei 8 jijini Dar es Salaam, ilifanya mkutano mkubwa wa hadhara Misima, ambapo umati wa wanchi ulihudhuria, huku kero nyingi zikiwasilishwa na kudhihirisha changamoto za utawala bora zinazoathiri maendeleo ya Tanzania.

Wakizungumza kwa uchungu mkubwa, mwananchi wa Misima aliyejitambulisha kwa jina la Mhina Ally, alisema viongozi wa Halmashauri kwa kushirikiana na madiwani waliamua kuingiza kijiji chao katika Halmashauri ya Mji bila ya kuwashirikisha, ikiwamo kubandika tangazo la pingamizi kwa siku 90 katika maeneo yao kama sheria inavyotaka.

Alisema kutoka Handeni Mjini hadi katika eneo lao ni kilomita 16 zilizozunguukwa na mapori yanayowafanya wananchi wajihusishe na kilimo kwa asilimia 99, hivyo kuingizwa kwenye sheria za mji ni kusababisha ugumu wa maisha.

“Inashangaza mno kusikia Tanzania kuna utawala bora wakati viongozi wachache wanaweza kufanya watakavyo; hali inayoweza kuleta mapigano makubwa, endapo wananchi tutasimama kidete kudai haki zetu zinazokandamizwa na viongozi kila siku,” alisema.

Ally alifika mbali zaidi kwa kusema walisikia tangazo redioni la kuingizwa kwenye Halmashauri ya Mji, huku tangazo la pingamizi likishindwa kuwekwa kijijini kwao kwa hofu ya kupingwa na wananchi wao.

“Viongozi wa serikali ya kijiji waliamua kutoliweka tangazo la pingamizi kijijini kwetu kwasababu wanajua fika tusingekubali, hivyo inashangaza malalamiko yetu kufumbiwa macho na serikali inayoitwa sikivu, licha ya kuzunguuka sehemu nyinyi, kama kwa Mkuu wa wilaya na Mkuu wa Mkoa wa Mkoa Tanga, alipokaimu DC Halima Dendego, ambaye sasa amekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara,” aliongeza.

Naye Naye Idd Kisege alisema kuwa ili kuona viongozi wanaogopa kufika Misima, hata namba kwenye nyumba zao hakuna ingawa wanatangaza uchaguzi kwa sheria za mji katika kijiji chao, jambo lisiloweza kuvumiliwa na kila mpenda maendeleo ya Misima.

“Watu wa Misima tunaambiwa sisi ni watata, wakorofi tunapodai haki zetu, ili waendelee kutuburuza, ndio maana kwenye ziara ya Mheshimiwa Rais, Profesa Jakaya Mrisho Kikwete waliniburuza Polisi kwasababu ya kuonyesha bango kwa mheshimiwa ili kuona kero zetu,” alisema Kisege.

Naye Mkomwa Athuman alisema kuwa Misima haipo tayari kutumikia sheria za Mji kwakuwa ni mapema mno kwao, hivyo wanaomba serikali, ikiwamo ofisi ya Waziri kulifuatilia suala hilo kwa kina.

“Mzozo huu umeshakuwa mkubwa na kuondoa ushirikiano kabisa kwa viongozi na wananchi wa hapa Misima, hivyo tayari malalamiko yetu yamefikishwa Ofisi ya Waziri Mkuu kulishtakia suala hilo kwasababu sheria ya kuingia kwenye Mamlaka ya Mji Handeni haijafuatwa na imeanzishwa na watu wachache ili kuzima uozo wa ardhi waliyoufanya kwenye kijiji chetu,” alisema.

Katika kila mwananchi aliyezungumza kwenye mkutano huo alionyesha kuguswa na kero hiyo ya mji, huku wakisema kutoka Handeni Mjini hadi Misima ni mbali pamoja na viongozi kushindwa kufuata sheria za utawala bora.

Awali, mkutano huo ulioanza saa tisa alasiri ulifunguliwa na mtoa mada wa kwanza, Kambi Mbwana, ambaye ndiye Msemaji Mkuu wa taasisi hiyo, aliyejikita sababu na dhamira kuu ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo.

Mbwana alisema kuwa sababu kubwa ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo ni kutoa elimu ya uraia na kuhamasisha utawala bora, ikiwa ni njia moja wapo ya kuwafanya Watanzania wote wajiletee maendeleo kwa kushirikiana baina yao na viongozi wote.

Akizungumzia utawala bora, Makamu Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Adam Malinda, alisema kwamba matatizo mengi katika jamii yamekuwa yakichangiwa na viongozi wasiojua nini maana ya utawala bora.

“Utawala bora ni somo muhimu na lazima lipigiwe kelele na watu wote, maana malalamiko mengi ya watu wa Misima yamesababishwa na tatizo hilo, ndio maana unaona kero zimepamba moto,” alisema.

Malinda aliwataka viongozi wa juu, wakiwamo wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni kuzungumza na wananchi wa Misima ili kutatua mtafaruku huo kwa ajili ya kuwafanya wananchi waendelee na shughuli za kujiletea maendeleo, sambamba na serikali kuwafanyia kazi watendaji wabovu.

Kuhusiana na mzozo huo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Handeni, Thomas Mzinga, alikaririwa akisema kuwa utaratibu ulifuatwa, ikiwamo kutoka kwa siku 60 za pingamizi, ingawa wananchi hao walishindwa kupita njia hiyto kwa ajili ya kufanikisha malengo yao.



Monday, November 10, 2014

SIWEZI KUVUMILIA:Kwanza soka lichezwe, jezi wakati mwingine

Na Kambi Mbwana, Handeni
WAZEE wa zamani walikuwa na makusudi yao kuweka msemo usemao sikio la kufa halisikii dawa. Na wakati mwingine wanasema siku ya kufa nyani miti yote huteleza. Misemo hii na mingine mingi inaelezea namna gani hutokea matatizo yanayokosa jinsi ya kuyatatua.


Ninaposema hili, najikuta nikikosa hamu ya kusikiliza au kusikia porojo zinazoitwa kuendeleza soka la Tanzania, chini ya Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF),  Jamal Malinzi. Malinzi aliyeingia madarakani hivi karibuni akirithi mikoba ya Leodgar Tenga, amekuwa akikabiliwa na matizo mengi, kiasi cha kuamini kuwa sikio la kufa halisikii dawa.


Hakika siwezi kuvumilia; TFF eti inajaribu kuangalia namna ya kuboresha jezi za timu ya Taifa, Taifa Stars. Sasa jezi zinasaidia nini? Hata tukivaa jezi za aina gani, kama hatuna soka zuri tunanufaika na kitu gani?


Huu ni ubabaishaji uliyoje? Malinzi na jopo lake kubwa analoteua kila uchao anapaswa kuwa makini mno ili asiharibu mwenendo wake mzuri. Kinyume cha hapo ni hasara tupu. Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo iliwahi kutangaza mchakato wa vazi la Taifa. Hadi leo haijulikani mchakato huo umeishia wapi?


Eti mshindi wa jezi ya nyumbani atapewa Sh Milioni moja kama atakavyopewa mshindi atakayebuni jezi za ugenini. Huku ni kupotezeana muda. Hizo Milioni 2 kama zipo TFF si alete mashindano japo ya Kata au wilaya?


Hizo Milioni 2 zinaweza kununulia vifaa vya michezo na kuwapa vijana wanaopenda kucheza soka ili hali hawana vifaa vya michezo? Hakika siwezi kuvumilia. Kwa upande wangu sikuwa na hamu kabisa ya kumlaumu Malinzi. Lakini kadri muda unavyosonga mbele kunafanyika matatizo yanayovunja ukimya.


Au pia wakati mchakato huo unaundwa, pengine kumeshapatikana mshindi na kuna kitu kinataka kufanywa. Malinzi, jezi hazina manufaa kwa sasa. Wala usisimbuke kuzibadilisha au kuziboresha maana zipo.


Watanzania wanataka soka safi. Soka la kuvutia litakalotupandisha chati na kuwaita mawakala wa Kimataifa kwa ajili ya wachezaji wetu. Huu ndio ukweli unaonifanya nishindwe kuvumilia mchana na usiku.


Kinyume cha hapo, utendaji kazi wa TFF ya sasa ni kuboresha jezi na kuhama ofisi kama vile mambo hayo hayakuwapo kabla ya uongozi wao.


Tuonane wiki ijayo.

+255712053949

NSSF yalibeba upya tamasha la Handeni Kwetu 2014



Na Mwandishi Wetu, Handeni
SHIRIKA la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii NSSF Tanzania, limejitokeza tena kudhamini Tamasha kubwa la Utamaduni linalojulikana kama ‘Handeni Kwetu’, lililopangwa kufanyika Desemba 13 mwaka huu, katika Uwanja wa Azimio (Kigoda Stadium), wilayani Handeni, mkoani Tanga.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Huduma kwa Wateja kutoka Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) Eunice Chiume, pichani.
Hii ni mara ya pili kwa mfuko huo wa hifadhi kudhamini tamasha hili la utamaduni lilioanza mwaka jana, ambapo lilifanyika kwa mafanikio makubwa kwa kushirikisha vikundi vya ndani na nje ya Handeni, wakiwamo wa jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia hilo, Mratibu Mkuu wa Tamasha hilo, Kambi Mbwana, alisema kujitokeza kwa NSSF ni kitendo cha kiungwana kinacholiweka tukio lao katika kiwango kizuri na mafanikio makubwa.

Alisema kwa kuliangalia hilo, wameamua kutoa haki ya jina, ambapo sasa tamasha lao litakuwa linajulikana kama NSSF Handeni Kwetu, wakiamini kuwa ni ishara nzuri ya ushirikiano baina yao na wadau wote wa shirika hilo.

“Yapo mashirika mengi Tanzania bila kusahau kampuni ambazo zingeweza kudhamini matukio ya aina hii ambayo yana mchango mkubwa kwa taifa letu, lakini baadhi yao yamekuwa magumu mno kudhamini au hata kuyasaidia kwa namna moja ama nyingine.

“Shirika kama NSSF linapoamua kuingia kudhamini ni kuonyesha jinsi wanavyoithamini jamii yao, jambo ambalo kwetu sisi ni furaha kubwa na kuona ipo haja ya kutafuta namna ya kurudisha fadhira kwa wadau hawa muhimu nchini Tanzania,” alisema.

Kwa mujibu wa Mbwana, siku ya tamasha, kutakuwa na shughuli ya kusajili wanachama wapya wa kujiunga na NSSF, ili waweze kunufaika na huduma za mafao kwenye Shirika hilo kubwa la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii hapa nchini.

Wadhamini wengine wa tamasha hilo ni pamoja na Phed Trans, SmartMind & Partners iliyopo chini ya Anesa Co. Ltd kwa kupitia kitabu cha ‘Ni Wakati wako wa kung’aa, Handeni Kwetu Foundation, Wait & Watch Film Company Ltd, Qs Mhonda J Apex Group of Companies Ltd na Skyblue Security and Risk Mgt Ltd na Michuzi Media Group.


Monday, November 03, 2014

Yusuphed Mhandeni alipigia chapuo tamasha la Handeni Kwetu


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MDAU wa muziki wa dansi Tanzania ambaye pia ni Mchumi wa Chama Cha Mapinduzi CCM, Kata ya Makumbusho, Yusuphed Mhandeni, amesema kuna haja kubwa wadau kuliunga mkono tamasha la Handeni Kwetu linalotarajiwa kufanyika Desemba 13, wilayani Handeni, mkoani Tanga ili kuchochea kasi ya maendeleo na kukuza uchumi wa nchi.
Mdau wa muziki wa dansi Tanzania, Yusuphed Mhandeni, pichani.
Akizungumza mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Mhandeni alisema kitendo cha kufanyika tamasha hilo na mengineyo makubwa Tanzania,si tu kinachangia kwa kiasi kikubwa kuitangaza sanaa na utamaduni wa Mtanzania, bali pia kunaleta maendeleo makubwa.
Alisema  tamasha la Handeni linafanyika katika eneo ambalo wananchi wake na viongozi kwa kiasi kikubwa wanapambania maendeleo, hivyo ni jambo la busara kuendelea kubuni matukio makubwa, sanjari na kushirikiana kwa kiasi kikubwa.
Mhandeni alisema nyumba za wageni, hoteli, migahawa na vyombo vya usafiri vinafanya biadhara kubwa kutoka kwa wananchi wanaohudhuria tamasha hilo, wakiwamo wasanii na vikundi vingi vinavyonufaika kwa uwapo wa tamasha hilo.
“Naungana na Watanzania wazalendo wakiwamo waandaaji wa tamasha kubwa la Handeni Kwetu, linaloandaliwa chini ya mratibu wake mkuu Kambi Mbwana, huku likipangwa kufanyika Desemba 13 mwaka huu wilayani Handeni mkoani Tanga kwasababu napenda maendeleo ya nchi yetu.
“Wengine waliunge mkono wakiwamo wafanyabiashara wakubwa, mashirika na kampuni mbalimbali za Tanzania kwa ajili ya kufaninisha maendeleo ya Taifa letu, ukizingatia kuwa ili tusonge mbele tunapaswa kuunga mkono juhudi kama hizi,” alisema Mhandeni.
Mhandeni ni miongoni mwa wadau wanaolipigia chapuo tamasha la Handeni Kwetu kwa kupitia mabasi yake ya Phed Trans yanayokwenda Mkata, wilayan Handeni, bila kusahau  SmartMind & Partners iliyopo chini ya Anesa Co. Ltd kwa kupitia kitabu chao cha Ni Wakati wako wa Kung’aa, Handeni Kwetu Foundation, Wait & Watch Film Company Ltd, Qs Mhonda J Apex Group of Companies Ltd na Skyblue Security and Risk Mgt Ltd.
Tamasha la Handeni Kwetu ni miongoni mwa matukio makubwa ya kiburudani mkoani Tanga, ambako zaidi ya watu 500 walihudhuria tamasha hilo ambalo kwa mwaka huu mipango kabambe ya kuhakikisha kuwa linafanyika kwa mafanikio.




LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...